• HABARI MPYA

  Ijumaa, Septemba 20, 2019

  AVEVA NA KABURU WANYIMWA DHAMANA BAADA YA DPP KUWASILISHA KUSUDIO LA KUPINGA UAMUZI WA MAHAKAMA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi, Kisutu mjini Dar es Salaam imewanyima dhamana kwa waliokuwa viongozi wa Simba SC, Rais Evance Elieza Aveva na Makamu wake, Geoffrey Hiliki Nyange ‘Kaburu’ 
  Uamuzi huo umekuja leo kufuatia Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama hiyo kuondoa mashtaka ya utakatishaji Fedha kwa Aveva na Kaburu.
  Na uamuzi huo ulitolewa wakati washitakiwa hao wamekwishafikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba kwa ajili ya kukamilisha masharti ya dhamana ili waweze kuachiwa huru. 
  Baada ya DP kuwasilisha kusudio la kupinga uamuzi wa Mahakama hiyo kuwaondolea mashtaka ya utakatishaji Fedha Aveva na Kaburu, sasa hatima ya dhamana ya wawili hao itajulikana Jumatatu kesi hiyo itakaposikilizwa tena.
  Ikumbukwe jana Mahakama ilisema Aveva na Kaburu wako huru kuwekewa dhamana baada ya kuondolewa mashitaka mawili ya utakatishaji fedha, kati ya 10 yanayowakabili.
  Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu mjini Dar es Salaam, Thomas Simba jana aliwapa masharti ya dhamana wawili hao baada ya kuwaondolea mashitaka ya utakatishaji fedha ambayo kwa mujibu wa sharia hayana dhamana.
  Akisoma uamuzi huo mahakamani hapo jana, Hakimu Simba alisema upande wa mashitaka unatakiwa kuthibitisha mashtaka yote kwa washitakiwa na kila shitaka linatakiwa kuthibitishwa peke yake pasipo kutegemeana.
  Alisema baada ya kupitia kwa makini na kuuchambua kwa kina ushahidi wa mashahidi 10 wa upande wa mashitaka wameamua kuyaondoa mashitaka namba tano, sita na 10 na kuwatia hatiani washitakiwa kwa mashitaka mengine saba, namba 1, 2, 3, 4, 7, 8 na 9, hivyo shitaka la utakatishaji limeondolewa.
  Wakili wa washtakiwa hao Nehwmia Nkoko aliiomba mahakama kuwapatia wateja wake dhamana baada ya mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo yaliyokuwa yanawanyima dhamana kuondolewa.
  Na jana Wakili wa Takukuru, Leornad Swai alipoulizwa kama anapingamizi lolote juu ya dhamana alidai hawana pingamizi na ndipo Hakimu Simba akawapa masharti Aveva na Kaburu kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh. Milioni 30 kwa kila mmoja pamoja na kuwa na vitambulisho
  Wawili hao walikuwa wanatuhumiwa kwa jumla ya makosa 10 yakiwemo ya utakatishaji ila upande wa mashtaka umeshindwa kudhibitisha mashtaka hayo ya utakatishaji.
  Mashitaka hayo 10 yalikuwa ni pamoja na ya kula njama, matumizi mabaya na kughushi nyaraka ikionyesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa Dola za Marekani 300,000 kwa Aveva kitu ambacho si kweli.
  Wanadaiwa kwamba  Machi 10 na 16, 2016, Aveva na Nyange waliandaa nyaraka za kuhamisha dola za kimarekani 3000,000 kutoka kwenye akaunti ya klabu ya Simba kwenda kwenye akaunti ya Aveva wakijua kuwa wanachofanya ni kosa.
  Pamoja na Aveva na Kaburu, mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Zacharia Hans Pope ambaye yeye yupo nje kwa dhamana na amekuwa akihudhuria mahakamani kila anapohitajika ikiwemo leo.
  Lakini Aveva na Kaburu walioingia madarakani Juni 30, mwaka 2014, hawakufanikiwa kumalizia muda wao madarakani, kufuatia kuwekwa rumande katika gereza la Keko tangu Juni 29, mwaka 2017 kwa tuhuma za kesi inayowakabili sasa mahakamani.
  Julai 1, mwaka huo, viongozi waliobaki katika Kamati ya Utendaji, Wajumbe Iddi Kajuna, Said Tully, Collins Frisch, Ally Suru na Jasmine Badour waliteua watu wa kukaimu nafasi za Aveva na Kaburu.
  Hao ni Mjumbe ni Mteule wa Kamati ya Utendaji, Salum Abdallah ‘Try Again’ aliyeteuliwa Kukaimu Urais na Kajuna Umakamu ambao walifanikiwa kuitisha uchaguzi mwingine Novemba 5, mwaka 2018 uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere mjini Dar es Salaam, Swedi Nkwabi akishinda Uenyekiti.
  Hata hivyo, Septemba 14, mwaka huu Mkwabi ameamua kujiuzulu wadhifa huo miezi 10 na ushei tu tangu achaguliwe akisema sababu ya kuchukua uamuzi huo ni kwamba mambo si shwari ndani ya klabu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AVEVA NA KABURU WANYIMWA DHAMANA BAADA YA DPP KUWASILISHA KUSUDIO LA KUPINGA UAMUZI WA MAHAKAMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top