• HABARI MPYA

  Jumapili, Septemba 22, 2019

  STARS YAJIWEKA PAGUMU KIDOGO KUFUZU CHAN BAADA YA KUCHAPWA 1-0 NA SUDAN LEO DAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TANZANIA imejiweka katika mazingira magumu ya kufuzu Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) mwakani nchini Cameroon baada ya kufungwa 1-0 nyumbani leo na Sudan katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya pili na ya mwisho ya mchujo kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, bao lililoizamisha Tanzania limefungwa na Yasir Mozamil dakika ya 60 akimalizia mpira uliourudi baada ya kugonga mwamba kufuatia shuti lake mwenyewe awali akimalizia krosi ya Ramadhan Agab aliyefanikiwa kumtoka beki wa kulia, Boniphace Maganga.


  Sasa Tanzania wanatakiwa kwenda kushinda 2-0 ugenini kwenye mchezo wa marudiano ambao Sudan wameomba ufanyike mjini Kampala, Uganda Oktoba 18 kwa sababu ya machafuko yanayoendelea nchini mwao.
  Sudan inayofundishwa na kocha wa zamani wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Mcroatia Zdravko Logarusic walipata pigo dakika ya 32 baada ya kiungo wake Mohammed Alrashed kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Nazar Hamid.
  Pamoja na kufungwa katika mchezo huo, Taifa Stars inayofundishwa na kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije ilicheza vyema na kutengeneza nafasi kadhaa, lakini kwa mara nyingine tena tatizo likawa katika umaliziaji. 
  Peke yake, mshambuliaji aliyerejea Azam FC ya nyumbani baada ya msimu mmoja wa kuwa na Tenerife nchini Hispania alipoteza nafasi nzuri za kufunga dakika ya saba, 19 na 85.
  Nao Ayoub Lyanga, Miraji Athuman ‘Madenge’ na Idd Suleiman ‘Nado’ pia walilijaribu lango la Sudan sawa na mabeki Maganga na Gardiel Michael kwa mashuti ya mbali, lakini sifa zimuendee kipa Ali Abdallah aliyeokoa.
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa: Juma Kaseja, Gardiel Michael, Boniphace Maganga, Erasto Nyoni, Kelvin Yandani, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Shaaban Iddi Chilunda, Ayoub Lyanga/Miraji Athuman dk67, Muzamil Yassin/Hassan Dilunga dk72, Jonas Mkude na Idd Suleiman ‘Nado’. 
  Sudan; Ali Abdallah, Abuaagla Abdallah, Amir Kamal, Abdallatif Saeed, Ramadhan Agab, Mohammed Al Rashed/Nazar Hamid dk32, Yasir Mozamil/Hussein Morsal dk89, Atahir Eltahir, Ahmed Mahmoud/Maaz Abdelrahim dk76, Nasreldin Omer na Ahmed Adam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: STARS YAJIWEKA PAGUMU KIDOGO KUFUZU CHAN BAADA YA KUCHAPWA 1-0 NA SUDAN LEO DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top