• HABARI MPYA

  Jumatano, Septemba 25, 2019

  MTIBWA SUGAR YAENDELEZA UNYONGE LIGI KUU, YAPIGWA 3-1 NA TANZANIA PRISONS MOROGORO

  Na Mwandishi Wetu, MOROGORO
  TIMU ya Mtibwa Sugar imeendelea kufanya vibaya katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya leo kuchapwa mabao 3-1 nyumbani na Tanzania Prisons Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
  Huo unakuwa mchezo wa nne mfululizo mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu wanacheza bila ushindi, wakifungwa tatu, nyingine 3-1 na Lipuli na 2-1 na Simba SC na kutoa sare moja, 0-0 na JKT Tanzania, ingawa zote za awali ugenini. 
  Katika mchezo wa leo, mabao ya Tanzania Prisons yamefungwa na Benjamini Asukile dakika ya 13, Samson Mbangula dakika ya 34 na Jeremiah Juma dakika ya 90, wakati la Mtibwa Sugar limefungwa na Issa Kaija dakika ya 56.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Hassan Kabunda dakika ya 39 limeipa KMC ushindi wa kwanza wa msimu, 1-0 dhidi ya Namungo FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
  Nao JKT Tanzania wakapata ushindi wa kwanza wa msimu, tena ugenini wakiichapa Biashara United 1-0, bao pekee la Mohamed Rashid dakika ya 16 Uwanja wa Karume mjini Musoma.
  Bao la dakika ya 90 na ushei likainusuru Ruvu Shooting kulala nyumbani kwa kupata sare ya 1-1 na Coastal Union ya Tanga iliyotangulia kwa bao la Menzi Chili dakika ya 60 Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  Na Uwanja wa Mwadui Complex, bao la Martin Kigi dakika ya 80 likainusuru Mwadui FC kupoteza mechi, ikipata sare ya 1-1 pia na jirani zao, Alliance FC ya Mwanza iliyotangulia kwa bao la Venance Ludovick dakika ya 57.
  Uwanja wa Namfua mkoani Singida, wenyeji Singida United wamelazimishwa sare ya 0-0 na Mbao FC ya Mwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MTIBWA SUGAR YAENDELEZA UNYONGE LIGI KUU, YAPIGWA 3-1 NA TANZANIA PRISONS MOROGORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top