• HABARI MPYA

  Alhamisi, Septemba 26, 2019

  SIMBA SC YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI LIGI KUU, YAICHAPA KAGERA SUGAR 3-0 KAITABA

  Na Mwandishi Wetu, BUKOBA
  SIMBA SC imeanza mapema utawala katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba jioni ya leo.
  Kwa ushindi huo uliotokana na mabao mawili ya mshambuliaji wake wa kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere na beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Simba SC sasa inafikisha pointi tisa kufuatia kushinda mechi zake zote tatu za mwanzo.
  Maana yake, Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick J Aussems ndiyo inaongoza Ligi Kuu kufuatia Lipuli FC kupunguzwa kasi leo baada ya sare ya 2-2 na Mbeya City mjini Iringa leo.


  Katika mchezo wa leo, Kagere alifunga bao la kwanza dakika ya 14 akimalizia kwa kichwa krosi ya winga wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Deo Kanda anayecheza kwa mkopo Msimbazi kutoka TP Mazembe ya kwao.
  Nahodha Msaidizi wa klabu na beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ akaifunga timu yake ya zamani dakika ya 35 akimalizia pasi ya Kagere.
  Kagere aliye katika msimu wake wa pili Simba SC tangu awasili kutoka Gor Mahia ya Kenya akafunga bao la tatu la Wekundu wa Msimbazi kwa penalti dakika ya 78.
  Kikosi cha Kagera Sugar kilikuwa; Said Kipao, Mwaita Gereza, David Luhende, Hassan Isihaka, Erick Kyaruzi/Juma Nyoso dk46, Zawadi Mauya, Awesu Awesu, Ally Ramadhani, Evarigestus Mjwahuki, Abdallah Seseme na Yussuf Mhilu/Peter Mwalyanzi dk50.
  Simba SC;  Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Tairone Santos, Serge Wawa, Gerson Fraga ‘Viera’, Deo Kanda/Miraj Athuman dk62, Muzamil Yassin, Meddie Kagere/Wilker Da Silva dk87, Sharaf Eldin Shiboub na Ibrahim Ajibu/Hassan Dilunga dk71.
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Lipuli FC wamelazimishwa sare ya 2-2 na Mbeya City Uwanja wa Samora mjini Iringa. Mabao ya Lipuli FC yamefungwa Issa Rashid dakika ya 15 na Paul Nonga dakika ya 77, wakati ya Mbeya City yamefungwa na George Chota dakika ya 47 na Ibrahim Mwakamole dakika ya 86.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI LIGI KUU, YAICHAPA KAGERA SUGAR 3-0 KAITABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top