• HABARI MPYA

  Ijumaa, Septemba 20, 2019

  ALLIANCE FC NA BIASHARA UNITED ZAFIKISHA MECHI TATU KILA TIMU BILA USHINDI LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  TIMU ya Alliance FC leo imeshindwa kutumia vizuri fursa ya kucheza nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Biashara United ya Musoma mkoani Mara Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza.
  Mshambuliaji mkongwe wa kimataifa wa Tanzania, Jerson John Tegete alianza kuwafungia Alliance FC dakika ya 11, akimalizia pasi ya Sameer Vincent, kabla ya  Innocent Edwin kuwasawazishia Biashara United dakika ya  45.
  Huo unakuwa mchezo wa tatu mfululizo kwa kila timu kucheza bila ushindi, Alliance wakitoa sare ya 1-1 na Mbao FC kabla ya kufungwa na Kagera Sugar 2-1 mjini Mwanza.

  Nao Biashara United waliuanza msimu kwa kufungwa 2-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Karume mjini Musoma kabla ya kuchapwa 1-0 na Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. 
  Ligi Kuu ya Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea kesho kwa mechi tano kuchezwa kwenye viwanja tofauti nchini.
  Namungo FC na Mwadui FC Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, JKT Tanzania na Mtibwa Sugar Uwanja wa Meja Isamuhyo huko Mbweni, nje kidogo ya Dar es Salaam, Ndanda FC na Singida United Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Mbeya City na Ruvu Shooting Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Mbao FC dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ALLIANCE FC NA BIASHARA UNITED ZAFIKISHA MECHI TATU KILA TIMU BILA USHINDI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top