• HABARI MPYA

  Jumatatu, Septemba 30, 2019

  TIMU TISA ZILIZOWAHI KUTWAA TAJI ZAFUZU HATUA YA MAKUNDI LIGI YA MABINGWA

  WANAUME wametenganishwa na wavulana, hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya kukamilika kwa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwishoni mwa wiki.
  Na sasa upangaji wa makundi manne ya timu nne kila moja kwa ajili ya hatua hiyo inayoshirikisha jumla ya timu 16 utafuatia Jumatano ya Oktoba 9 mjini Cairo, Misri.
  Miongoni mwa timu zilizofuzu hatua hyo ni pamoja tisa zilizowahi kubeba taji hilo kubwa la klabu Afrika angalau mara moja, wakiwemo mabingwa watetezi Esperance ya Tunisia. 
  ‘Damu na Dhahabu’ wamefuzu baada ya kuitoa Elect Sport ya Chad, wakitoka nyuma kwa mabao 2-1 na kushinda 3-2 jumla na kupata tiketi ya kucheza kwa mara ya nne mfululizo hatua ya makundi.

  Wanaungana na ndugu zao, Etoile du Sahel, ambao licha ya kumaliza na wachezaji 10 walipindua kipigo cha 2-0 katika mechi ya kwanza dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana kwa kushinda 3-0 mjini Monastir na kufuzu.
  Mabingwa wa Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns, washindi wa mwaka 2016 walipata ushindi mkubwa wa 11-1 dhidi ya vibonde, Cote d’Or ya Seychelles, ambao unakuwa ushindi mkubwa zaidi kihistoria kwenye michuano hiyo, hivyo ‘Wabrazil’ hao kuendeleza rekodi yao ya kuingia hatua ya makundi mfululizo tangu 2016.
  Wababe wawili wa Morocco, Raja Club Athletic na Wydad Athletic Club, wote mabingwa wa zamani, wamefuzu pia wakikutana tena kwenye hatua hiyo tangu 2011 walipofuzu pamoja kwa mara ya mwisho. Wydad walifika hadi fainali na kufungwa 1-0 na Esperance 1-0.
  Baada ya miaka nane ya kukosekana, JS Kabylie ya Algeria, mabingwa wa 1981 na 1990 wamerejea hatua ya makundi, wakiungana na mahasimu wao, USM Alger waliofungwa kwenye fainali ya mwaka 2015.
  Mabingwa mara tano, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) walkuwa wana kazi nyepesi kwa Fosa Juniors ya Madagascar wakishnda 3-1 na kufuzu kwa mara ya tatu mfululizo hatua ya makundi, wakungana na mahasimu wao, AS Vita mabingwa wa 1973 kutinga hatua hiyo.
  Mabingwa wa rekodi, mara nane Al Ahly ya Misri wamefuzu hatua ya makundi kwa mara ya tano mfululizo baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya Cano Sport ya Equatorial Guineans na kufuzu kwa ushindi wa jumla wa 6-0.
  Mbali na mabingwa hao wa zamani, timu nyingine zilizofuzu hatua hiyo ni mahasmu wa Angola, Petro Atletico na Primeiro de Agosto, El Hilal ya Sudan, FC Platinum ya Zimbabwe na Zesco United ya Zambia.
  Nafasi ya mwisho baina ya Zamalek ya Misri na Generation Foot ya Senegal itaamuliwa baada ya kikao cha bodi ya Shirikisho la Soka Afrka (CAF) hivi karibuni.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TIMU TISA ZILIZOWAHI KUTWAA TAJI ZAFUZU HATUA YA MAKUNDI LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top