• HABARI MPYA

    Monday, September 02, 2019

    SAMATTA ALIMWA KADI YA NJANO, ATOLEWA GENK IKITOA SARE NA CLUB BRUGGE UBELGIJI

    Na Mwandishi Wetu, BRUGGE
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana alionyeshwa kadi ya njano kabla ya kupumzishwa, timu yake KRC Genk ikilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Club Brugge katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Jan Breydel mjini Brugge.
    Samatta alionyeshwa kadi hiyo dakika ya 85 katika mchezo ambao wenyeji walitangulia kwa bao la beki Muivory Coast, Simon Deli dakika ya 41 akimalizia pasi ya kiungo Mholanzi Ruud Vormer, kabla ya Genk kusawazisha kupitia kwa beki Sebastien Dewaest dakika ya 67 akimalizia pasi ya Mbelgiji mwenzake, Bryan Heynen.
    Pamoja na Samatta aliyetolewa dakika ya 90 na ushei kumpisha mshambuliaji mpya, Mnigeria Ebere Paul Onuachu aliyesajiliwa kutoka Midtjylland ya Denmark, wengine walioonyeshwa kadi za njano na refa Erik Lambrechts ni Piotrowski dakika ya 23 , Okereke dakika ya 45 na ushei, Berge dakika ya 56, Ndongala dakika ya 80 na Dennis dakika ya 92.
    Mshambuliaji wa KRC Genk, Mbwana Samatta (kulia) akijaribu kumpita beki wa Club Brugge jana Uwanja wa Jan Breydel mjini Brugge 

    Jana Kwa Samatta mwenye umri wa miaka 26 amecheza mechi ya 162 kwenye mashindano yote tangu amejiunga na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa amefunga mabao 67 jumla.
    Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 128 na kufunga mabao 52, kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili, katika Super Cup mechi moja na Europa League mechi 24 katika mabao 14.
    Kikosi cha Club Brugge kilikuwa: Mignolet, Diatta, Okereke/Openda dk84, Deli, Ricca/Sobol dk73, Vanaken, Vormer, Rits, Tau/Dennis dk71, Mechele na Mata.
    KRC Genk: Coucke, De Norre, Dewaest, Lucumi, Uronen, Berge, Heynen, Piotrowski/Hrosovsky/45, Ito, Paintsil/Ndongala dk62 na Samatta/Onuachu dk94.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA ALIMWA KADI YA NJANO, ATOLEWA GENK IKITOA SARE NA CLUB BRUGGE UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top