• HABARI MPYA

  Ijumaa, Januari 26, 2018

  SANKHANI MKANDAWIRE AWAVURUGA MBEYA CITY, ASAINI MIAKA MIWILI MALAWI NA HUKU ANA MKATABA HADI MWAKANI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Mbeya City imepata pigo kufuatia beki wake anayeweza kucheza kama kiungo pia, Sankhani ‘Mkango Plus’ Mkandawire kurejea kwao Malawi na kujiunga tena na klabu yake, Big Bullets.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu kutoka Mbeya leo, Katibu Mkuu wa Mbeya City FC, Emmanuel Kimbe amesema kwamba wameona picha na nakala za magazeti Mkandawire akisaini BB.
  Hata hivyo, Kimbe amesema kwamba Mkandawire amewadanganya Big Bullets kwamba huku hakuwa na mkataba wakati ukweli ni kwamba mkataba wake unaisha Juni mwaka 2019.
  Sankhani ‘Mkango Plus’ Mkandawire (kulia) akisaini mkataba wa kurejea Big Bullets nchini Malawi juzi 
  Amesema wakati anajiunga na Mbeya City Juni mwaka juzi alisaini mkataba wa miaka mitatu ambao unamalizika Juni mwakani.
  Kimbe alisema mchezaji huyo aliondoka wiki iliyopita akiomba ruhusa anakwenda kwao kuna msiba na akaahidi kurejea Jumatatu ya Januari 29.
  Na kuhusu madai kwamba mchezaji huyo ameamua kuvunja mkataba kwa sababu hajapewa mishahara ya miezi mitano Mbeya City, Kimbe amesema ni kweli. 
  “Si kweli. Sankhani anadai mshahara wa mwezi mmoja tu huu tulionao wa kwanza. Mshahara wa Desemba (2017) ulichelewa ukatoka wakati amekwenda Malawi na amewekewa. Tuseme mikononi mwetu kuna mishahara yake ya miezi miwili,”amesema Kimbe.
  Zaidi ya hapo, Kimbe amesema kwamba Sankhani pia anadai sehemu ya ada ya kusaini ambayo katika makubalino ya mkataba wa miaka mitatu ni awe anapewa kwa awamu, jambo ambalo hata mchezaji mwenyewe analielewa.
  “Sisi tumeona hizo nakala za magazeti na tunazo kama ushahidi. Tunasubiri ruhusa yake iishe (Jumatatu), asipotokea tunaandika barua TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) kuwashitaki klabu na mchezaji mwenyewe,”amesema Kimbe.
  Nchini Malawi, magazeti mbalimbali yameripoti Mkandawire amerejea Nyasa Big Bullets kwa kusaini mkataba wa miaka miwili akitokea Mbeya FC alikodumu kwa miaka miwili.
  Mkandawire amesaini kwa ada Kwacha Milioni 2 na mshahara wa Kwacha 250 000 kwa mwezi akiungana na wachezaji wengine wapya waliosajiliwa mwezi huu, Righteous Banda kutoka Civil Sporting Club, Patrick Phiri kutoka Premier Bet Wizards na Precious Phiri kutoka Azam Tigers.
  The Nation limeandika mchezaji huyo amesema kwamba amevunja mkataba na Mbeya City kwa makubalino na klabu hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SANKHANI MKANDAWIRE AWAVURUGA MBEYA CITY, ASAINI MIAKA MIWILI MALAWI NA HUKU ANA MKATABA HADI MWAKANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top