• HABARI MPYA

  Alhamisi, Januari 25, 2018

  AZAM FC WAMKATAA REFA NKONGO KUWACHEZESHA DHIDI YA YANGA JUMAMOSI CHAMAZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo umeandika barua rasmi kwenda Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) inayoelekea kutokuwa na imani na mwamuzi Israel Nkongo.
  Mwamuzi huyo ndiye amepangwa kuchezesha mchezo ujao wa Azam FC dhidi ya Yanga, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex keshokutwa Jumamosi saa 10.00 jioni.
  “Kama klabu, itakumbukwa kuwa mechi zetu ambazo mwamuzi huyu (Nkongo) amekuwa akizichezesha zimekuwa na malalamiko mengi na utata mwingi juu ya maamuzi ya uwanjani,” ilisema moja ya nukuu kwenye barua hiyo.
  Barua hiyo ilizidi kueleza kuwa moja ya sababu nyingine ya kumlalamikia mwamuzi huyo na kukosa imani naye, ni kitendo chake cha kuzua utata mkubwa kwenye mchezo aliochezesha mkoani Mbeya wiki moja iliyopita kati ya Tanzania Prisons na Mbeya City kutokana na uamuzi wake.
  Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohamed, aliyeandika barua hiyo na kutuma nakala kwa Kamati ya Waamuzi, TFF na Yanga, ameweka wazi kuwa kwa kuzingatia uzito wa mchezo huo wameiomba bodi hiyo kubadilisha mwamuzi kwa kumpanga mwingine.
  Aidha katika barua hiyo, Mohamed ameongeza kuwa kutokana na timu zote mbili kutoka katika mkoa wa Dar es Salaam, ameiomba bodi hiyo kumpanga mwamuzi ambaye atatoka nje ya mkoa huo.
  Mbali na Nkongo kupangwa kuchezesha mchezo huo, waamuzi wengine waliopangwa kushirikiana naye ni Josephat Bulali atakayekuwa mwamuzi msaidizi namba moja, msaidizi namba mbili atakuwa Soud Lila, mwamuzi wa akiba ni Elly Sasii huku Omar Abdulkadir akiwa Kamishna wa mchezo huo, wote wakitoka Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC WAMKATAA REFA NKONGO KUWACHEZESHA DHIDI YA YANGA JUMAMOSI CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top