• HABARI MPYA

  Ijumaa, Januari 26, 2018

  YANGA BADO WASOTEA KIBALI CHA LWANDAMINA, NSAJIGWA PIA KUKOSEKANA KESHO MECHI NA AZAM FC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC bado inasotea kibali cha kufanyia kazi cha kocha wake, Mzambia George Lwandamina kuelekea mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC kesho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Ofisa Habari wa Yanga SC, Dissmas Ten amesema kwamba taratibu za kupata kibali cha Lwandamina zinaendelea na matarajio hadi jioni ya leo wanaweza kuwa wamefanikiwa.
  “Kuhusu suala la kibali cha Mwalimu (Lwandamina), tayari kimefanyiwa kazi na taratibu zote zimeshafuatwa, hivyo mashabiki na wanachama waondoe shaka juu ya jambo hilo,” amesema Ten.
  Yanga SC bado inasotea kibali cha kufanyia kazi cha kocha wake, Mzambia George Lwandamina  

  Aidha, Ofisa Habari huyo amesema kwamba kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Azam FC, Yanga itawakosa wachezaji wake saba ambao ni mabeki Pato Ngonyani, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, viungo Pius Buswita, Thabani Kamusoko na washambuliaji Amissi Tambwe, Yohana Nkomola na Donald Ngoma.
  Wote watakosekana kwa sababu ni majeruhi, wakati kiungo Pius Buswita yeye hatakuwepo kwa sababu anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.
  Pamoja na hayo, Ten amesema wachezaji waliobaki wanaweza kabisa kuisaidia timu kuibuka na ushindi katika mchezo huo wa ugenini wa kukamilisha duru la kwanza la Ligi Kuu. 
  Wakati huo huo: Kocha Msaidizi wa Yanga, Nsajigwa Shadrack Mwandemele hatakuwepo kesho kwa sababu amefiwa na shemeji yake, hivyo amekwenda kuzika.
  Ni Kocha wa mazoezi ya viungo pekee, Mzambia mwingine, Noel Mwandila ambaye yuko tayari kuingoza timu kwa mchezo wa kesho hadi sasa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA BADO WASOTEA KIBALI CHA LWANDAMINA, NSAJIGWA PIA KUKOSEKANA KESHO MECHI NA AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top