• HABARI MPYA

  Alhamisi, Januari 25, 2018

  RUVU SHOOTING YAPANIA KUCHUKUA POINTI TATU KWA MBAO FC KESHO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Ruvu Shooting imepania kushinda mechi dhidi ya Mbao FC kesho Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba timu imekuwa katika maandalizi mazito tangu wamalize mchezo wao uliopita ambao walifungwa 1-0 na Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Bwire amesema kwamba baada ya matokeo hayo yasiyoridhisha benchi la Ufundi chini ya kocha Mkuu, Abdulmutik Hajji ‘Kiduu’ anayesaidiwa na Suleiman Mtungwe walikwenda kufanyia kazi mapungufu.
  Ruvu Shooting imepania kuifunga Mbao FC kesho Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani

  Amesema walimu wamefanya kazi kubwa na nzuri katika kipindi hiki na sasa vijana wapo tayari kwa mchezo wa kesho na matarajio ni ushindi. 
  Bwire amesema kwamba jambo jema zaidi ni kwamba kikosini hakuna mchezaji majeruhi, mgonjwa wala mwenye adhabu ya kadi za kumkosesha mechi ya kesho.
  Na amesema wanatarajia upinzani mkali kutoka kwa Mbao FC kwa kuwa ni timu nzuri na ina wachezaji wazuri, lakini watapambana washinde tu.
  Hali mbaya Ruvu Shooting, ikiwa inashika mkia katika Ligi Kuu misimu miwili tu warejee kutoka Daraja la Kwanza baada ya kuambulia pointi 11 katika mechi 14 walizocheza.  Duru la kwanza la Ligi Kuu linakamilishwa wikiendi hii na mbali na Ruvu Shooting kuwa wenyeji wa Mbao FC kesho, Jumamosi Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Njombe Mji FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na Azam FC wataikaribisha Yanga SC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Mechi nyingine za Jumamosi, Mbeya City watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Sokoine mjini na Kagera Sugar wataialika Lipuli FC Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
  Mechi nyingine zitachezwa Jumapili, vinara wa ligi hiyo, Simba SC watamenyana na Maji Maji FC ya Songea na Singida United watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Namfua mkoani Singida. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: RUVU SHOOTING YAPANIA KUCHUKUA POINTI TATU KWA MBAO FC KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top