• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 31, 2018

  SAMATTA AREJEA NA PASI YA BAO GENK YAFUNGWA 3-2 KOMBE LA UBELGIJI

  Na Mwandishi Wetu, GENK
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta jana ametoa pasi ya bao la kwanza la timu yake, KRC Genk ikifungwa 3-2 na wenyeji, Kortrijk katika mechi ya Kombe la Ubelgiji Guldensporen mjini Kortrijk.
  Samatta alimsetia mshambuliaji Marcus Ingvartsen kuifungia bao la kwanza Genk dakika ya 17, kabla ya kiungo Mnigeria, Abdul Ajagun kuwasawazishia wenyeji dakika ya 23 na kiungo mwingine, Mfaransa Larry Azouni akafunga la pili dakika ya 36.
  Wakati kipindi cha kwanza kikikaribia kabisa kumalizika, Genk wakasawazisha kupitia kwa kiungo Mbelgiji, Thomas Buffel dakika ya 45 na ushei.
  Kipindi cha pili, wenyeji, Kortrijk wakamaliza kazi kwa lao tatu la beki Mfaransa, Lucas Rougeaux dakika ya 88 na sasa timu hizo zitarudiana Februari 6 nyumbani kwa Genk, Luminus Arena.
  Jana Samatta alikuwa anacheza kwa mara ya pili tangu apone maumivu ya mishipa midogo ya goti lake la mguu wa kulia iliyochanika Novemba 4, mwaka jana akiichezea KRC Genk ikilazimishwa sare ya 0-0 na Lokeren katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk na kumsababisha afanyiwe upasuaji mdogo. 
  Mechi ya kwanza ni iliyopita iliyokuwa ya Ligi, ambayo aliingia dakika saba za mwisho kuchukua nafasi ya Mkosovo Edon Zhegrova, Genk ikilazimishwa sare ya 1-1 na Sint-Truiden Januari 27 Uwanja wa Luminus Arena kabla ya jana kuanza hadi dakika ya 75 alipompisha Zhegrova.
  Samatta jana amecheza mechi ya 72 Genk tangu alipojiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Na katika mechi hizo 70, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mashindano yote.
  Kikosi cha KV Kortrijk kilikuwa; Kaminski, Kumordzi, Makarenko, Kagelmacher, Rougeaux, Ajagun/Verboom dk9, Chevalier/Perbet dk77, Van Der Bruggen, Azouni/De Smet dk71, Ouali na D'Haene.
  KRC Genk; Vukovic, Uronen, Colley, Dewaest, Nastic, Wouters, Seck, Malinovskyi/Writers dk77, Samatta/Zhegrova dk75, Buffel na Ingvartsen/Vanzeir dk62.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA AREJEA NA PASI YA BAO GENK YAFUNGWA 3-2 KOMBE LA UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top