• HABARI MPYA

  Jumatatu, Januari 29, 2018

  AISHI MANULA ADAKA MECHI 14 BILA KURUHUSU BAO KATI YA 20 TANGU ATUE SIMBA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MLINDA mlango Aishi Salum Manula jana amedaka mechi ya 20 tangu ajiunge na Simba SC Julai mwaka jana kutoka Azam FC, lakini kitu cha kuvutia zaidi ni kwamba amefikisha mechi 14 za kudaka bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa Msimbazi.
  Simba jana imeibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Maji Maji ya Songea mkoani Ruvuma katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ushindi huo, unaifanya Simba SC imalize duru la kwanza la Ligi Kuu na pointi 35 baada ya kucheza mechi 15, ikiwazidi kwa pointi saba mabingwa watetezi, Yanga walio nafasi ya tatu na pointi tano, Azam FC wanaoshika nafasi ya pili. 
  Aishi Manula jana amedaka mechi ya 20 tangu ajiunge na Simba SC zikiwemo 14 za kudaka bila kufungwa 

  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Erick Onoka wa Arusha, aliyesaidiwa na washika vibendera Mohammed Mkono wa Tanga na Anold Bugado wa Singida, mabao ya Simba SC yalifungwa na washambuliaji, Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ kipindi cha kwanza na Mganda Emmanuel Anord Okwi kipindi cha pili, kila mmoja mawili.
  Lakini langoni Aishi alikuwa ana biashara tofauti, kuzuia mipira isiingie kwenye nyavu za Simba na akafanikiwa kumaliza dakika 90 nyingine bila kufungwa.
  Maana yake kipa huyo mwenye umri wa miaka 22 aliyeibukia kwenye akademi ya Azam FC amefikisha mechi 14 za kudaka bila kufungwa, nyingine zikiwa ni dhidi ya Rayon Sport katika Simba Day Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ikishinda 1-0, sare ya 0-0 katika mchezo wa kirafiki na Mlandege FC Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Akadaka kwa dakika zote 90 bila kufungwa katika sare ya 0-0 na Yanga kwenye mechi ya Ngao ya Jamii na kwenda kuisaidia timu kushinda kwa penalti 5-4, akadaka Simba ikishinda 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, sare ya 0-0 na Azam FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na ushindi wa 3-0 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Taifa zote za Ligi Kuu.
  Akadaka katika sare ya 0-0 na wenyeji, Milambo kwenye mchezo wa kirafiki Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, ushindi wa 4-0 dhidi ya Njombe Mji Uwanja wa Uhuru, 1-0 mfululizo dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na 2-0 dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara zote zikiwa mechi za Ligi Kuu.
  Mechi nyingine ni Simba ikishinda 4-0 dhidi ya Singida United Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na na ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba za Ligi Kuu.
  Aishi, kipa namba moja wa taifa, ameokoteshwa mipira katika mechi sita ambazo ni katika sare ya 2-2 na Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ushindi wa 2-1 dhidi ya Stand United Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, sare nne za 1-1 Uwanja wa Uhuru dhidi ya Mtibwa Sugar, Yanga, Lipuli FC za Ligi Kuu pia na 1-1 dhidi ya  Green Warriors Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  Green Warriors walifanya maajabu baada ya kuwafunga Simba waliokuwa mabingwa watetezi kwa penalti 4-3 baada ya sare hiyo ya 1-1 ndani ya dakika 90. 
  Ni wiki mbili zilizopita tu Aishi Manula aliposogeza jiko ndani, baada ya kufunga pingu za maisha na mpenzi wake wa siku nyingi, Aisha.
  Aishi Manula akiuwahi mpira dhidi ya mshambuliaji wa Yanga Donald Ngoma kwenye mechi ya Ngao ya Jamii Agosti mwaka jana

  REKODI YA AISHI MANULA SIMBA SC
  Simba 1-0 Rayon Sport (Hakufungwa Kirafiki Simba Day Taifa)
  Simba 0-0 Mlandege FC  (Hakufungwa Kirafiki Amaan, Zbar)
  Simba 0-0 (5-4 penalti) Yanga (Hakufungwa Ngao ya Jamii, Taifa Penalti)
  Simba 7-0 Ruvu Shooting (Hakufungwa Ligi Kuu Uhuru)
  Simba 0-0 Azam FC (Hakufungwa Ligi Kuu Chamazi)
  Simba  3-0 Mwadui (Hakufungwa Ligi Kuu Uhuru)
  Simba  2-2 Mbao FC (Alifungwa mbili Ligi Kuu Kirumba, Mwanza)
  Simba 0-0 Milambo (Aliingia, hakufungwa Kirafiki A. Mwinyi, Tabora)
  Simba 2-1 Stand United (Alifungwa moja Ligi Kuu Shinyanga)
  Simba  1-1 Mtibwa Sugar (Alifungwa moja Ligi Kuu Uhuru)
  Simba  4-0 Njombe Mji (Hakufungwa Ligi Kuu Uhuru)
  Simba 1-1 Yanga (Alifungwa moja Ligi Kuu Uhuru)
  Simba 1-0 Mbeya City (Hakufungwa Ligi Kuu Sokoine)
  Simba 1-0 Tanzania Prisons (Hakufungwa Ligi Kuu Sokoine)
  Simba 1-1 Lipuli FC (Alifungwa moja Ligi Kuu Uhuru)
  Simba 1-1 (Penalti 3-4) Green Warriors (Alifungwa moja na penalti nne Kombe la TFF Chamazi)
  Simba 2-0 Ndanda FC (Hakufungwa Ligi Kuu Nangwanda)
  Simba 4-0 Singida United  (Hakufungwa Ligi Kuu Uhuru)
  Simba 2-0 Kagera Sugar  (Hakufungwa Ligi Kuu Kaitaba)
  Simba 4-0 Maji Maji FC (Hakufungwa Ligi Kuu Taifa)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AISHI MANULA ADAKA MECHI 14 BILA KURUHUSU BAO KATI YA 20 TANGU ATUE SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top