• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 24, 2018

  MWASHIUYA AREJEA YANGA IKIJIANDAA KUIVAA AZAM, NKOMOLA…

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WINGA wa Yanga SC, Geoffrey Mwashiuya amerejea kuongeza nguvu kikosini kuelekea mechi na Azam FC wikiendi hii.
  Azam FC wataikaribisha Yanga SC Jumamosi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuhitimisha duru la kwanza. 
  Na kuelekea mchezo huo, pamoja na kurejea kwa Mwashiuya, lakini kocha Mzambia wa Yanga, George Lwandamina anasikitika anaweza kumkosa mshambuliaji chipukizi, Yohanna Oscar Nkomola.
  Geoffrey Mwashiuya (kulia) amerejea kuongeza nguvu kikosini kuelekea mechi na Azam FC wikiendi hii

  Nkomola alishindwa kumalizia mechi hiyo dhidi ya Ruvu Shooting Jumapili baada ya kutolewa dakika  ya 28 kufuatia kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Emmanuel Martin.
  Lwandamina amesema kwamba pamoja na Nkomola, majeruhi wengine wapya ni beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Pato Nonyani na kiungo mshambuliaji, Pius Buswita ambaye pia hawezi kucheza dhidi ya Azam FC kwa sababu ya anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.  
  “Orodha ya majeruhi inaongezeka, tunazidi kuwa katika wakati mgumu, lakini hatuna namna zaidi ya kuendelea kupambana hivyo hivyo,”amesema Lwandamina.
  Majeruhi wengine Yanga ni Wazimbabwe kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donaldo Ngoma ambao Lwandamina amesema hana matumaini ya kuwapata kabisa msimu huu.
  Yanga SC inazidiwa pointi tano na Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya vinara, Simba SC wenye pointi 32 na Jumamosi itahitaji kupunguza gepu hilo.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MWASHIUYA AREJEA YANGA IKIJIANDAA KUIVAA AZAM, NKOMOLA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top