• HABARI MPYA

    Saturday, January 27, 2018

    WACHEZAJI FRIENDS RANGERS WAFUNGIWA KWA KUGEUZA SOKA NDONDI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MCHEZAJI wa Friends Rangers, Almasi Mkinda amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumpiga ngumi mchezaji wa African Lyon katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 14, 2018 Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
    Adhabu hiyo katika mechi namba 44 Kundi A Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, African Lyon wakishinda 2-1, ni kwa mujibu wa Kanuni ya 37 (3) ya Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
    Nao wachezaji Mtoro Hamisi wa Friends Rangers, na Prosper Mushi wa African Lyon wamefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kila mmoja baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kupigana uwanjani. Adhabu imezingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.

    Bosi wa Friends Rangers, Heri Mzozo timu yake inakabiliwa na changamoto ya nidhamu

    Daktari wa Friends Rangers, Rajabu Shabani amefungiwa miezi mitatu na kupigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kuwatolea lugha ya matusi na dharau waamuzi wa mechi hiyo. Adhabu imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 41(2) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Viongozi.
    Klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kuonyeshwa kadi zaidi ya tano katika mechi hiyo. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 42(10) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
    Mechi namba 45 Kundi A (JKT Tanzania 5 v African Lyon 1). Klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa kukiuka Kanuni ya 14(13) kutokana na kugoma kuingia vyumbani katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 20, 2018 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ulioko Mbweni jijini Dar es Salaam. Adhabu dhidi ya klabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Nayo JKT Tanzania imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuingia eneo la kuchezea kushangilia ushindi. Klabu hiyo imeadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
    Mechi namba 41 Kundi B (JKT Mlale 1 v Mawenzi Market 0). Daktari wa Mawenzi, Novatus Ngowi amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya kuwatolea waamuzi lugha isiyokuwa ya kiungwana katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 13, 2018 kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
    Mechi namba 43 Kundi B (Mbeya Kwanza 0 vs KMC 0). Kocha wa Mbeya Kwanza, Maka Mwalwisi amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kuzungumza na waandishi wa habari baada ya mechi hiyo iliyochezwa Januari 13, 2018 Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kumalizika akiwashambulia viongozi wa TFF akidai wanaandaa timu za kupanda Ligi Kuu, ndiyo maana waamuzi wananyonga haki yao ya kupata ushindi.
    Mechi namba 47 Kundi B (Polisi Tanzania 0 vs Coastal Union 0). Klabu ya Polisi Tanzania imepigwa faini ya jumla ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na gari la washabiki wa timu hiyo kuingia uwanjani, na kuzunguka uwanja wakati timu zikifanya mazoezi. Pia wakati wa mapumziko na baada ya mchezo kumalizika washabiki wa timu hiyo waliwafuata waamuzi na kutaka kuwapiga.
    Vilevile washabiki wa timu hiyo walitoa lugha chafu kwa viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA) katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 20, 2018 Uwanja wa Ushirika mjini Moshi. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
    Mechi namba 44 Kundi C (Biashara United 2 vs Alliance Schools 0). Klabu ya Alliance Schools imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na timu yake kutoingia vyumbani katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 13, 2018 katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Mechi namba 45 Kundi C (JKT Oljoro 1 vs Dodoma FC 1). Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Emmanuel Muga na Mwamuzi wa Akiba, Gilbyrth Mrina wamepata alama za chini hivyo kukosa sifa ya kuendelea kuchezesha Ligi.
    Hivyo, Kamati imeteua wajumbe watatu kupitia mkanda wa mechi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine itachunguza kiwango cha uchezeshaji cha waamuzi kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi dhidi yao.
    Mechi namba 47 Kundi C (Biashara United 1 vs Rhino Rangers 1). Daktari wa Viungo wa Rhino Rangers, Ahamad Mgongo na kipa Mohamed Ibrahim Salumu wa Rhino Rangers wamesimamishwa hadi suala lao la utovu wa nidhamu waliofanya litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF. Wamesimamishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) ya Ligi Daraja la Kwanza.
    Mbali ya kumpiga teke Msimamizi Msaidizi wa Kituo cha Mara, Mgongo pia wakati vurugu zikiendelea katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 21, 2018 Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma alimchapa kibao Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Athuman Rajabu.
    Naye kipa Salumu baada ya kumuangusha kwa makusudi ndani ya eneo la hatari mchezaji wa Biashara United, na refa kuamuru adhabu ya penalti dhidi yake alimpiga ngumi kwa makusudi mchezaji huyo wa Biashara United. Baada ya vurugu kutulia Mwamuzi alimuonyesha kadi nyekundu. Lakini Kipa huyo baada ya kuamuliwa kutoka nje alimpiga Mwamuzi ngumi ya kisogoni.
    Mechi namba 48 Kundi C (Transit Camp 0 vs Alliance Schools 3). Wachezaji Mohamed Suleiman Ussi, Khalid Mahmud Konobile, Abubakar Ramadhan na Victor William Alimwene wa Transit Camp wamepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumkimbilia Mwamuzi baada ya mechi kumalizika kwa lengo la kumfanyia vurugu kabla ya askari polisi kuingilia kati.
    Walifanya kitendo hicho katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 21, 2018 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
    Wakati huo huo: Mchezaji Gideon Joram Richard wa The Mighty Elephant anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kitendo chake cha kwenda karibu na chumba cha waamuzi baada ya mechi na kuwakashfu kuwa ni mabwege katika mchezo namba 21 Kundi C Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara dhidi ya Burkina Faso uliomalizika kwa sare ya 2-2 Januari 15 Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WACHEZAJI FRIENDS RANGERS WAFUNGIWA KWA KUGEUZA SOKA NDONDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top