• HABARI MPYA

  Alhamisi, Januari 25, 2018

  NDANDA FC YAIKANYANGA STAND UNITED 1-0 PALE PALE KAMBARAGE

  Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
  TIMU ya Ndanda FC imefanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji, Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga jioni ya leo.
  Pongezi kwake mfungaji wa bao hilo pekee, Omar Mponda dakika ya 81 katika mchezo huo uliokuwa mgumu kutokana na kila timu kupigania ushindi kwa bidii.
  Baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, kila timu ilibadilisha maarifa kipindi cha pili Stand wakitaka kuendeleza wimbi la ushindi, wakitoka kushinda ugenini 1-0 dhidi ya Mbao FC mjini Mwanza huku Ndanda wakitaka kuondoka Shinyanga bila kupoteza mechi baada ya kutoa sare na Mwadui kwenye mchezo uliopita.
  Lakini bahati ilikuwa ni ya timu kutoka Kusini mwa Tanzania hii leo, Ndanda FC wakiwazima wenyeji wao kwa bao la dakika za mwishoni.
  Kwa ushindi huo, Ndanda FC inafikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi 15 na kupanda hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wakiishusha Mbao FC ambayo inaweza kurudi juu yao ikishinda dhidi ya Ruvu Shooting Mlandizi kesho.
  Stand United inabaki nafasi ya 13 kwa pointi zake 13 za mechi 15, ikiwa juu ya Kagera Sugar, Njombe Mji FC zenye pointi 12 kila moja na Ruvu Shooting yenye ponti 11, ingawa zenyewe zina mechi moja moja mkononi. 
  Mzunguko wa 15 wa Ligi Kuu utaendelea kesho kwa mechi moja tu, Ruvu Shooting wakiwa wenyeji wa Mbao FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani wakati Jumamosi Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Njombe Mji FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na Azam FC wataikaribisha Yanga SC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Mechi nyingine za Jumamosi, Mbeya City watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Kagera Sugar wataialika Lipuli FC Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, wakati Jumapili, vinara wa ligi hiyo, Simba SC watamenyana na Maji Maji FC ya Songea na Singida United watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Namfua mkoani Singida. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NDANDA FC YAIKANYANGA STAND UNITED 1-0 PALE PALE KAMBARAGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top