• HABARI MPYA

  Ijumaa, Januari 26, 2018

  SANCHEZ ADAIWA KUKWEPA VIPIMO DAWA ZA KUONGEZA NGUVU

  WAKATI mshambuliaji mpya, Alexis Sanchez anatarajiwa kuanza kuichezea Manchester United leo dhidi ya Yeovil kwenye mechi ya Kombe la FA England, taarifa zinasema Mchile huyo hakufanya vipimo vya dawa za kuongeza nguvu zilizopigwa marufuku michezoni.
  Sanchez alitarajiwa kufanyiwa vipimo hivyo Jumatatu kwenye viwanja vya mazoezi vya Arsenal, lakini siku hiyo tayari alikuwa Manchester kukamilisha uhamisho wake.
  Haifahamiki nani mwenye makosa kati ya Sanchez, anayejiunga na Manchester United kwa mshahara wa Pauni 600,000 kwa wiki, au Arsenal aambayo inaweza kuadhibiwa.
  Lakini pia kuna utata kama Maofisa wa vipimo hivyo vya dawa za kuongeza nguvu zisizoruhusiwa michezoni walifika viwanja vya mazoezi vya Arsenal, Colney London.

  Alexis Sanchez anadaiwa kukwepa vipimo vya dawa zilizopigwa marufuku michezoni 

  Taarifa za awali nchini Hispania zimesema wapimaji kutoka Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) waliwasili na kuomba sampuli za Sanchez ili tu kugundua hakuwepo, lakini UEFA oAlhamisi ilikanusha kuhusika katika hilo.
  Zaidi inaonekana kwamba Sanchez alifanya makosa kusafiri kwenda kukamilisha uhamisho wake United wakati taarifa zake za wapi alipo zilikuwa zinaonyesha yupo London. 
  FA na Arsenal walikataa kuzungumzia hilo Alhamisi na ni vigumu kusema nani mwenye makosa. Klabu zinatakiwa kuandaa taarifa za wapi wanapofanyia mazoezi - mchezaji gani atakuwa anafanya mazoezi na kikosi gani - lakini kwenye Ligi Kuu ya England ni wajibu wa mchezaji mwenyewe kutoa taarifa za wapi alipo. 
  Kama mwenyewe, mchezaji anaweza kuadhibiwa kwa kufungiwa hadi miaka miwili kama atatafutwa mara tatu bila kupatikana ndani ya mwaka mmoja lakini haifahamiki kama hii ni mara ya kwanza, ya pili au ya tatu kwa ama Sanchez au Arsenal.
  Adhabu si kubwa kwa klabu,  mwaka jana Manchester City ilipigwa faini ya Pauni 35,000na kupewa onyo baada ya kuvunja sheria za vipimo vya dawa zisizoruhusiwa michezoni kwa kushindwa kutoa taarifa wapi walipo mara tatu ndani ya miezi 12.
  Sanchez anatarajiwa kuanza kuichezea United leo katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Yeovil na hadi sasa hakuna aliyewasiliana na Mashetani hao Wekundu kati ya FA na watu wa vipimo hivyo nchini Uingereza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SANCHEZ ADAIWA KUKWEPA VIPIMO DAWA ZA KUONGEZA NGUVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top