• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 24, 2018

  BAO LA DAKIKA YA MWISHO LAIONDOA RWANDA CHAN

  TIMU ya taifa ya Rwanda imetupwa nje ya michuano ya Ubingwa wa Mataifa wa Afrika (CHAN) baada ya kuchapwa bao 1-0 na Libya katika mchezo wa mwisho wa Kundi C usiku wa jana Uwanja wa Ibn Batouta mjini Tangier nchini Morocco.
  Libya ilipata bao lake dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho wakati tayari Rwanda wameanza kushangilia kwenda Robo Fainali, kwani sare ingewatosha kufikisha pointi tano na kumaliza nafasi ya pili Kundi C nyuma ya vinara, Nigeria. 
  Lakini Elmutasem Abushnaf aliyetokea benchi akazima ndoto hizo za Amavubi kwa kufunga bao hilo pekee la ushindi dakika ya 90.
  Nigeria imeongoza kundi hilo kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na Libya pointi sita, Rwanda inabaki na pointi zake nne na Equatorial Guinea inamaliza mikono mitupu baada ya kufungwa mechi zote.
  Nigeria imemaliza na ushindi wa 3-1 dhidi ya Equatorial Guinea jana Uwanja wa Agadir, mabao yake yakifungwa na Anthony Okpotu dakika ya 59, Dayo Ojo dakika ya 69 na Rabiu Ali kwa penalti dakika ya 83 huku la vibonde wao likifungwa na Nsi Eyama dakika ya 40.
  Nigeria inarejea Tangiers tayari kwa Robo Fainali na mshindi wa pili wa Kundi D, atakayejulikana leo na nafasi kubwa inapewa Angola inayomenyana na Kongo leo Uwanja wa Agadir. 
  Mechi nyingine ya mwisho ya Kundi D leo ni kati ya Burkina Faso na Cameroon Uwanja wa Ibn Batouta na zote zitaanza Saa 4:00 usiku.
  Timu zilizofuzu Robo Fainali hadi sasa ni Morocco, Sudan kutoka Kundi A, Zambia, Namibia Kundi B, Nigeria, Libya Kundi C na Kongo ya Kundi D.
  Msimamo wa Kundi D, Kongo inaongoza kwa pointi zake sita ikifuatiwa na Angola pointi nne, Burkina Faso pointi moja na Cameroon ambayo haina pointi.
  Ili Burkina Faso kwenda Robo Fainali, kwanza iombe Angola ifungwe na Kongo na yenyewe isifunge, (mfano Kongo 2-0, 1-0, Angola) hata bao moja na wao waifunge Cameroon si chini ya mabao 4-0 leo.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BAO LA DAKIKA YA MWISHO LAIONDOA RWANDA CHAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top