• HABARI MPYA

  Jumamosi, Januari 27, 2018

  YANGA WAIZIMA AZAM FC CHAMAZI…WAMEULIWA NA KIJANA WAO WENYEWE GARDIEL MICHAEL

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imeshindwa kutumia vyema Uwanja wa nyumbani baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 28 baada ya kucheza mechi 15, ingawa inaendelea kukaa nafasi ya tatu, nyuma ya Azam FC yenye pointi 30 na Simba SC pointi 32.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Israel Mujuni Nkongo aliyeyesaidiwa na washika vibendera Soud Lila na Frank Komba, hadi mapumziko tayari Yanga walikuwa wamekwishatengeneza ushindi wao huo.
  Lakini ilibidi Yanga watoke nyuma baada ya mshambuliaji chipukizi, Shaaban Iddi Chilunda kutangulia kuifungia Azam FC bao la kuongoza dakika ya nne tu akimalizia krosi ya Mzimbabwe, Bruce Kangwa aliyemtoka beki Hassan Kessy pembeni na kuingia ndani.
  Wachezaji wa Yanga wakimfuata Gardiel Michael aliyeinama kushangilia naye baada ya kufunga bao la pili
  Mfungaji wa bao la kwanza la Yanga, Obrey Chirwa akimtoka kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar 'Sure Boy'
  Beki wa Azam FC, Bruce Kangwa akigombea mpira na beki wa Yanga, Hassan Kessy
  Mfungaji wa bao la Azam FC, Shaaban Iddi akigeuka na mpira mbele ya beki wa Yanga, Andrew Vincent 'Dante'  
  Beki wa Yanga, Gardiel Michael akiokoa dhidi ya winga Mghana wa Azam FC, Enock Atta Agyei

  Mzambia Obrey Chirwa akaisawazishia Yanga dakika ya 30 baada ya kupokea pasi ya kiungo mshambuliaji, Ibrahim Ajib na kumpiga chenga kipa wa Azam, Mghana Razack Abalora aliyetoka bila maarifa ya ziada.
  Katika mastaajabu ya wengi, kocha wa Azam FC, Mromania Aristica Cioaba alimtoa mshambuliaji Mghana, Bernard Arthur aliyekuwa anacheza vizuri na kuwatia misukosuko mabeki wa Yanga, akamuingiza kiungo Salmin Hoza.
  Haikuwa ajabu Yanga walipouteka mchezo kwa kasi na mashambulizi mfululizo hadi wakafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 44 lililofungwa na beki Gardiel Michael Mbaga aliye katika msimu wake wa kwanza  Jangwani tangu asajiliwe kutoka Azam aliyefunga kwa shuti la umbali wa mita 30 baada ya pasi ya Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi.
  Ushangiliaji wa Gardiel kana kwamba alijua ndio bao la ushindi, lakini ulitosha kupeleka ujumbe kwa viongozi wa Azam FC kwamba walikosea kumuacha.
  Kipindi cha pili mchezo ulinoga zaidi, Azam FC wakisaka bao la kusawazisha na Yanga ambayo leo iliongozwa na kocha wake, Mzambia George Lwandamina ikitafuta bao la pili.
  Cioaba akasahihisha makosa yake baada ua kurudisha mshambuliaji uwanjani na kutoa kiungo, akimuingiza Mbaraka Yussuf kwenda kuchukua nafasi ya Stephan Kingue Mpondo.    
  Azam FC ilipata pigo dakika ya 79 baada ya kiungo wake, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu kufuatia kumchezea rafu beki wa Yanga, Hassan Kessy. Sure boy alionyeshwa kadi ya kwanza ya njano dakika ya 22 alipomchezea Emmanuel Martin.
  Kutoka hapo, Yanga wakauteka kabisa mchezo, lakini wakaishia kukosa mabao ya wazi tu.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mwadui FC imelazimishwa sare ya 2-2 na Njombe Mji FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Mbeya City imelazimishwa sarte ya 0-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Kagera Sugar imetoka 0-0 na Lipuli FC Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
  Kikosi cha AzamFC; Razack Abalora, Himid Mao, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Aggrey Morris, Stephane Kingue/Mbaraka Yussuf dk55, Joseph Mahundi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Bernard Arthur/Salmin Hoza dk36, Shaaban Iddi/Paul Peter dk62 na Atta- Agyei.
  Yanga SC; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Andrew Vincent, Kevin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, Raphael Daudi, Papy Kabamba Tshishimbi, Obrey Chirwa, Ibrahim Ajib/Juma Mahadhi dk68 na Emmanuel Martin/Geoffrey Mwashiuya dk62.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA WAIZIMA AZAM FC CHAMAZI…WAMEULIWA NA KIJANA WAO WENYEWE GARDIEL MICHAEL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top