• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 24, 2018

  MECHI YA AZAM NA YANGA NI SAA 10:00 JIONI CHAMAZI… REFA NI NKONGO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetaja viingilio vya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya wenyeji, Azam FC na Yanga SC Jumamosi wiki hii Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. 
  Taarifa ya TFF kwa vyombo vya Habari jioni ya leo imesema kwamba viingilio kwenye mchezo huo vitakuwa ni Sh 10,000 kwa Jukwaa Kuu na Sh. 7,000 kwa majukwaa ya kawaida. 
  Aidha, taarifa hiyo imesema kwamba huo mchezo huo namba 115, utaanza Saa 10:00 jioni Uwanja wa Azam Complex Chamazi. 
  Pamoja na hayo, TFF imetaja waamuzi watakaochezesha mechi hiyo wote ni kutoka Dar es Salaam ambao ni Israel Nkongo atakayesaidiwa washika vibendera ni Josephat Bulali na Soud Lila, wakati refa wa akiba atakuwa Elly Sasii na Kamishna wa mchezo huo ni Omar Abdulkadir. 
  Israel Nkongo (kulia) na Josephat Bulari (kushoto) wote watakuwa kazini Jumamosi Uwanja wa Azam Complex

  Mchezo namba 114 kati ya Mwadui FC ya Shinyanga na Njombe Mji ya Njombe uliokuwa ufanyike Ijumaa Januari 26, 2018 imesogezwa kwa siku moja kupisha mazishi ya aliyekuwa kocha msaidizi wa Mwadui Jumanne Ntambi na sasa utachezwa Jumamosi pia.
  Kocha huyo msaidizi wa Mwadui alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu kabla ya kufikwa na mauti.
  Kwa ujumla duru la kwanza la Ligi Kuu linafungwa wikiendi hii kwa mechi mzunguko wa 14, kuanzia Ijumaa Ruvu Shooting na Mbao FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Jumamosi Mwadui FC na Njombe Mji FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na Kagera Sugar na Lipuli ya Iringa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
  Mechi nyingine za Jumamosi ni kati ya Azam FC na Yanga SC Chamazi, Stand United na Ndanda FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mbeya City na Mtibwa Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Jumapili  Simba SC watakuwa wenyeji wa Maji Maji FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea na Singida United na Tanzania Prisons Uwanja wa Namfua, Singida. 
  Yanga SC inazidiwa pointi tano na Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya vinara, Simba SC wenye pointi 32 na Jumamosi itahitaji kupunguza gepu hilo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MECHI YA AZAM NA YANGA NI SAA 10:00 JIONI CHAMAZI… REFA NI NKONGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top