• HABARI MPYA

  Thursday, October 05, 2017

  YANGA KUCHEZA MECHI YA KIRAFIKI DHIDI YA KMC JUMAPILI CHAMAZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA wa Tanzania, Yanga SC watakuwa na mchezo wa kirafiki na KMC ya Kinondoni Jumapili Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Mchezo huo ni maalum kuwaweka fiti wachezaji wa timu hiyo kipindi hiki cha mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa zikiwemo za kirafiki na za kufuzu Kombe la Dunia.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu ya Yanga, Dissmas Ten ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba katika mchezo huo, mwalimu anatarajiwa kuwapa nafasi wachezaji ambao wamekuwa hawatumiki sana katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Aidha, Ten amesema kwamba kipa Beno Kakolanya aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu anatarajiwa kudaka kwa mara ya kwanza Jumapili msimu huu baada ya kupona.
  “Kakolanya amepona na yuko fiti kabisa kwa sasa, tunatarajia Jumapili utakuwa mchezo wake wa kwanza msimu huu tangu apone,”amesema.
  Ligi Kuu imesimama kwa siku 10 kupisha mechi za kimataifa zikiwemo za kirafiki na za kufuzu Kombe la Dunia na ikirejea, Oktoba 14 Yanga watakuwa wageni wa Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
  Katika mechi tano za awali za Ligi Kuu, Yanga imevuna pointi tisa kutokana na sare tatu na kushinda mbili, ikiwa inazidiwa pointi mbili na zote, Azam FC, Mtibwa Sugar na Simba zinazoongoza kwa pamoja.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA KUCHEZA MECHI YA KIRAFIKI DHIDI YA KMC JUMAPILI CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top