• HABARI MPYA

  Thursday, October 12, 2017

  TFF YAFUKUZA MAKOCHA WASIO NA VYETI TIMU ZA DARAJA LA KWANZA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BODI ya Ligi (TPLB) ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limewapiga marufuku makocha watano wa timu za Ligi Daraja la Kwanza kukaa katika mabenchi ya timu hizo kwa sababu ya kukosa sifa.
  Makocha hao ni Mathias Wandiba wa Pamba FC ya Mwanza, Salum Waziri wa JKT Mgambo ya Tanga, Adam Kipatacho wa African Lyon ya Dar es Salaam, Omba Thabit wa Mvuvumwa FC ya Kigoma na Ngelo Manjamba wa Polisi Dar.
  Makocha hao wamekuwa kwenye mabenchi ya timu wakifanya kazi kama makocha wakuu katika mechi nne mfululizo za Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2017/2018 inayoendelea hivi sasa.
  Kwa mujibu wa kanuni ya 72 (3) (5) ya Ligi Daraja la Kwanza, Kocha Mkuu anatakiwa kuwa na Leseni ya chini kuanzia daraja C ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) wakati Kocha Msaidizi anatakiwa kuwa na  sifa isiyopungua ngazi ya Kati cha Ukocha (Intermediate).
  Tayari Idara ya Ufundi ya TFF imefafanua wazi kuwa makocha hao hawana Leseni C ya CAF hivyo hawastahili kukaa kwenye mabenchi ya timu zao kama makocha wakuu.
  Vitendo vinavyofanywa na timu husika ni ukiukwaji wa kanuni, na ni matarajio ya TFF kuwa viongozi wa timu hizo watasitisha mara moja kwa makocha hao kukaa kwenye mabenchi ili kuepika adhabu.
  TFF tunachukua nafasi hii kuzikumbusha klabu husika kwamba kuanzia msimu ujao 2018/2019 kuwa sifa ya Kocha Mkuu wa kila timu ya Daraja la Kwanza ni Leseni B ya CAF.
  Katika hatua nyingine, baada ya mtihani wa utimamu wa mwili kwa waamuzi wenye beji za FIFA na wale wa Daraja la Kwanza kufanyika Agosti, 2017, sasa ni zamu ya waamuzi wa madaraja ya Tatu na Pili.
  Waamuzi wa madaraja ya Tatu na Pili kuanzia leo Alhamisi Oktoba 12, 2017 wameanza vipimo kabla ya  mitihani ya utimamu wa mwili katika vituo viwili vya Dar es Salaam na Mwanza.  
  Kwa wale watakaopata matokeo mazuri, watapata fursa ya kupandisha madaraja kwa mujibu wa utaratibu.
  Zoezi hilo litajumuisha pia wale waamuzi wa Daraja la Kwanza walioshindwa mitihani hiyo mwezi Agosti, mwaka huu. Hivyo nao wanaruhusiwa kwenda kufanya mitihani tena.
  Kituo cha Dar es Salaam kitakuwa na waamuzi wa mikoa ya Dar es Salaam yenyewe, Pwani, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya, Rukwa na Songwe.
  Kituo cha Mwanza kitakuwa na waamuzi wa mikoa ya Mwanza yenyewe, Mara, Kagera, Simiyu, Geita, Kigoma, Arusha, Shinyanga, Tabora, Dodoma, Singida, Manyara na Katavi.
  Waamuzi wote waende kwenye vituo vyao walivyopangiwa kama ilivyoelekezwa Oktoba 12, 2017 - ni siku ya kupima afya kabla ya kuanza kwa mitihani mingine ukiwamo wa utimamu wa mwili hapo kesho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF YAFUKUZA MAKOCHA WASIO NA VYETI TIMU ZA DARAJA LA KWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top