• HABARI MPYA

  Friday, October 06, 2017

  MANJI AACHIWA HURU KESI YA DAWA ZA KULEVYA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imemuachia huru Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Yanga, Yussuf Mehboob Manji katika kesi ya matumizi ya dawa za kulevya iliyokuwa inamkabili.
  Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha amesema leo mahakamani hapo kwamba upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka hayo dhidi ya Manji hivyo anaachiwa huru.
  Huo ni ushindi mwingine kwa mfanyabiashara huyo mwenye asili ya Kiasia, baada ya awali kuachiwa huru pia kwenye kesi ya uhujumu uchumi ambayo ilimfanya asote rumande kwa takriban miezi miwili.
  Manji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mbagala (CCM), aliachiwa huru baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha hati ikionyesha kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya bilionea huyo.
  Katika kesi ya Uhujumu Uchumi, Manji alikamatwa pamoja na wafanyakazi wake, Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda, Mtunza Stoo, Abdallah Sangey na Thobias Fwere.
  Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alimuambia Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa wameomba 'remove order' na kwamba Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) kwa niaba ya Jamhuri wanaiarifu Mahakama kwamba hakusudii kuendelea kuwashtaki Manji na wenzake katika kesi hiyo.
  Hivyo wanaomba kuiondoa kesi hiyo chini ya kifungu cha 91(1) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
  Baada ya misukosuko iliyodumu tangu mwishoni mwa mwaka jana, Manji sasa anaweza kurejesha nguvu zake katika uendeshaji wa kampuni zake, ingawa kuna changamoto nyingine pia zinazomkabili, ikiwemo madeni ya Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) yaliyosababisha baadhi ya ofisi zake kufungwa.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MANJI AACHIWA HURU KESI YA DAWA ZA KULEVYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top