• HABARI MPYA

  Sunday, October 01, 2017

  KAMA ANCELOTTI AMEFUKUZWA BAYERN MUNICH, LWANDAMINA YANGA…

  BAYERN MUNICH wameamua kuachana na kocha Mtaliano Carlo Ancelotti mara tu baada ya timu kufungwa mabao 3-0 na Paris Saint Germain kwenye mchezo wa Kundi B Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano mjini Paris.
  Katika taarifa yao rasmi, Bayern wamesema kwamba wameachana na kocha huyo mwenye umri wa miaka 58 kufuatia kikao cha ndani baada ya kipigo cha PSG katikati ya wiki.
  Aliyekuwa Msaidizi wa Ancelotti, Willy Sagnol sasa ndiye anaiongoza timu kwa muda, ingawa taarifa zinasema kocha wa Hoffenheim, Julian Nagelsmann anapewa nafasi kubwa ya mrithi wa kudumu wa Mtaliano huyo.
  Lakini pia, Mtendaji Mkuu wa klabu, Karl-Heinz Rummenigge amekuwa na majadiliano binafsi na kipenzi chake, kocha wa zamani wa Borussia Dortmund, Thomas Tuchel na kuna uwezekano kocha huyo akawa Mjerumani wa kwanza kuishika timu hiyo tangu kuondoka kwa Jupp Heynckes mwaka 2013.
  Rummenigge amesema katika taarifa yake kwenye tovuti ya Bayern Munich kwamba kiwango cha timu yao tangu mwanzoni mwa msimu hakijafikia matarajio waliyojiwekea na kwamba mechi ya Paris iliwaonyesha wazi wanapaswa kufanya maamuzi. 
  Amesema yeye na Mkurugenzi wa Usajili wa Bayern, Hasan Salihamidzic walizungumza na Carlo jana na kumjulisha uamuzi wao.
  Wanne kati ya wasaidizi wa Ancelotti - Wataliano wenzake, Davide Ancelotti (mtoto wa Carlo), Giovanni Mauri, Francesco Mauri na Mino Fulco - pia wameondoka Bayern. 
  Kocha huyo wa zamani wa Real Madrid na Chelsea, Ancelotti alianza kazi Bayern Julai mwaka 2016 akichukua nafasi ya Mspaniola Pep Guardiola aliyehamia Manchester City.
  Akaendeleza umwamba wa Bayern katika Bundesliga kwa kuiwezesha kubeba ubingwa ikiwa ina pointi 10 zaidi ya washindi wa pili, RB Leipzig. Pia ametwaa mataji ya Super Cup ya Ujerumani msimu huu na uliopita.
  Pamoja na hayo walifungwa 3-2 nyumbani katika Nusu Fainali ya Kombe la Ujerumani na Borussia Dortmund, na kwenye Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2016-2017 walifungwa na Real Madrid. Bayern haijashinda taji lolote la Ulaya tangu mwaka 2013. 
  Lakini kumekuwa na matatizo pia ndani na nje ya Uwanja - kipa namba moja Manuel Neuer ni majeruhi na ataendelea kuwa nje hadi baada ya Krisimasi na mbadala wake, Sven Ulreich ameshindwa kuziba pengo hilo vizuri, akifanya makosa na kufungwa bao la kwanza la kizembe dhidi ya Wolfsburg.
  Mshambuliaji tegemeo, Robert Lewandowski amelaumu sera ya ubakhili ya klabu akisema wanapaswa kutumia fedha zaidi kusajili huku pia mashabiki na vyombo vya habari wakilaumu Thomas Muller kutokupewa muda wa kutosha wa kucheza.
  Kusajiliwa kwa James Rodriguez kwa mkopo wa miaka miwili kumeleta mawazo tofauti, wakati kustaafu kwa Philipp Lahm na Xabi Alonso kumeuacha uongozi katika wakati mgumu. 
  Wakati Ancelotti anafukuzwa baada ya msimu mmoja tu, nchini England wamiliki wa klabu ya Manchester City sasa wanafurahia matunda ya kocha Mspaniola, Pep Guardiola katika msimu wake wa pili baada ya msimu mbovu wa kwanza.
  Man City ya msimu uliopita haikumfikirisha yoyote kama kigezo kingekuwa ni matokeo Guardiola angeingia katika msimu wa pili - lakini jana timu huyo imetoka kushinda mchezo uliofikiriwa mgumu dhidi ya mabingwa watetezi, Chelsea 1-0 ugenini Uwanja wa Stamford Bridge, London.
  Vyombo vya Habari vya Uingereza ambavyo msimu uliopita vilikuwa vinamkandia Guardiola, sasa vipo mstari wa mbele kumsifia – vikisema amewasuta (si ametusuta) waliokuwa (si tuliokuwa) wanamkandia msimu uliopita baada ya kupewa bajeti ya kusajili wachezaji awatakao.
  Na ni kweli, Guardiola alipoingia City hakuwafurahia aina ya wachezaji wengi waliokuwapo akapendekeza apewe bajeti ya kusajili nyota awatakao, na baada ya hapo, timu imekuwa moto.
  Ancelotti amefukuzwa kwa kufungwa PSG tena ugenini, timu ambayo mwaka jana ilikaribia kuwatoa Barcelona katika michuano hiyo hiyo, tena wakati huo hawana Neymar Junior wala Kylian Mbappe. Wengi wanaamini Barca alibebwa kuwatoa PSG msimu uliopita katika Ligi ya Mabingwa. 
  Wakati nastaajabu ya Bayern Munich na Ancelotti, hapa nyumbani kocha wa mabingwa wa Tanzania, Mzambia George Lwandamina amekwishaanza kupigiwa yowe za “aondoke” kufuatia timu kuambulia pointi tisa tu katika mechi tano za mwanzo za Ligi Kuu.
  Lwandamina alikuja Yanga Desemba mwaka jana, baada ya klabu kuvutiwa na mafanikio yake alipokuwa Zesco United ya kwao, alipoiongoza hadi Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Wakati huo huo, Yanga licha ya kufanikiwa kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, lakini haikufanya vizuri chini ya kocha wake, Mholanzi, Hans van der Pluijm hivyo uongozi ukaamua kuleta kocha mwenye rekodi nzuri kwenye michuano ya Afrika.
  Na matokeo mabaya ya mwanzoni mwa msimu uliopita yakawasaidia Yanga kupata sababu zaidi za kumuondoa Pluijm, ambaye kwa sasa yupo na Singida United. Yanga ikapatwa na anguko kubwa la kiuchumi kufuatia aliyekuwa Mwenyekiti na mfadhili wake, Yussuf Manji kupata matatizo na Serikali kabla ya kuamua kujiuzulu.
  Na hayo yalitokea wakati waliokuwa wadhamini wakuu wa klabu kwa takriban miaka nane, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wametoka kuondoka kufuatia kutofautiana na Manji. Yanga iliingia katika wakati mgumu mno, ikishindwa kulipa wachezaji na makocha mishahara hadi kusababisha migomo ya mara kwa mara.
  Pamoja na hayo, timu ikafanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu tu kutokana na ushindani mdogo uliokuwapo. Baada ya msimu, Yanga ikapata mdhamini mwingine mkuu, kampuni ya SportPesa na kidogo hali ikawa nzuri kifedha japo si kwa kiwango cha wakati wa Manji na TBL.
  Bado kumekuwa na migomo ya wachezaji mara kadhaa, wakilalamikia kutolipwa mishahara yao kwa muda mrefu na wakati wote wa kuwapo kwa Lwandamina, Yanga haijawahi kucheza soka ya kuvutia, huku viwango vya wachezaji wengi vikionekana wazi kushuka siku hadi siku.
  Wachezaji Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donald Ngoma ambao klabu ilitumia fedha kuwaongeza mikataba mwanzoni mwa msimu, wote hawapo katika ubora wao kabisa msimu huu.
  Washambuliaji wengine, Mrundi Amissi Tambwe na Mzambia, Obrey Chirwa wamekuwa majeruhi kwa muda mrefu msimu huu na katika wachezaji wapya hadi sasa ambao unaweza kusema wameingia na moto wao ni beki Gardiel Michael kutoka Azam na mshambuliaji Ibrahim Hajib kutoka Simba.
  Kwa kuitazama kwa nje na hata ndani, Yanga ina matatizo mengi sana yenye kukatisha tamaa, ambayo yanahitaji ufumbuzi wa haraka. Tumeona ambavyo Bayern Munich wamemuondoa Acelotti baada ya mwaka mmoja tu na ambavyo Man City walimvumilia Guardiola na sasa wanakula matunda yake katika msimu wa pili. Yanga wafanye nini? Watajua wenyewe, ila ninachoweza kusema; “Wana matatizo”.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAMA ANCELOTTI AMEFUKUZWA BAYERN MUNICH, LWANDAMINA YANGA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top