• HABARI MPYA

    Wednesday, July 08, 2015

    SIMBA, YANGA NA TFF WAIPITIE UPYA MIKATABA YAO NA TBL

    TIMU ya Free State Stars ya Bethlehem mwishoni mwa wiki imetwaa ubingwa wa vijana chini ya umri wa miaka 21 Afrika Kusini, maarufu kama SAB U21 Championship baada ya kuifunga Mpulamanga kwa penalti 3-1 kufuatia sare ya 1-1.
    Michuano hiyo ya saba ya U21 inayoandaliwa na Chama cha Soka Afrika Kusini (SAFA) chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Afrika Kusini (SAB), ilifanyika Uwanja wa Giant mjini Soshanguve.
    Na Free State ambayo imemsajili Mrisho Ngassa wa Tanzania Mei mwaka huu kutoka Yanga SC kwa ajili ya kikosi cha kwanza, imeweka historia kwa kuwa timu ya kwanza kutetea taji hilo. Haukuwa ushindi mwepesi kwa Free State kwani walilazimika kuifunga timu ambayo imetoa mfungaji bora na mchezaji bora wa mashindano, Siphamandla Dhlamini.
    Wasaka vipaji kadhaa walimiminika kwenye michuano hiyo ambayo imekuwa ikizalisha nyota kibao wa taifa hilo kusaka vipaji vya kupandisha Ligi Kuu.
    Pamoja na kudhamini mashindano hayo, SAB pia ina mchango mkubwa katika soka ya Afrika Kusini tangu mwishoni mwa miaka ya 1950. 
    Ilianza na kutumia bia ya Castle Lager kudhamini Ligi ya nchi hiyo mwaka 1959 na kwa sasa ni wadhamini wa timu ya taifa, Bafana Bafana, tangu nchi hiyo ipate uanachama wa FIFA. 
    SAB pia imekuwa ikisapoti michezo yote Afrika Kusini, ikiwemo kuchangia kwa kiasi kikubwa ufanisi wa Kombe la Dunia mwaka 2010 ambalo nchi hiyo walikuwa wenyeji.
    Afrika Kusini wanajivunia mno udhamini wa SAB katika soka yao, kwani imekuwa pia ikisapoti mashindano hadi ya vijana na ya kuibua vipaji.
    SAB pia ndiyo wamiliki wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambayo kwa hapa nchini si haba, wana mchango mkubwa nao katika soka yetu.
    Ni wadhamini wakuu wa timu ya taifa, Taifa Stars na klabu kongwe Simba na Yanga, zote za Dar es Salaam.
    Kwa muda mrefu nimekuwa nikidhani kwamba makampuni aina ya SAB yapo kibiashara zaidi na hayawezi kuwekeza fedha katika michezo ya vijana ambayo bado haina mashabiki wengi.
    Lakini kumbe ilikuwa dhana potofu, baada ya kugundua kwamba kwa mwaka saba sasa SAB wanadhamini michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 21 Afrika Kusini.
    SAB inafurahi kuona inachangia mchakato wa kuibua vipaji vya soka Afrika Kusini, ambayo mwishowe vinakuja kuwa tegemeo la taifa.
    Ndani ya miaka hiyo saba- SAB inajivunia kila kitu katika soka ya Afrika Kusini kwa sasa kutokana na mashindano hayo ambayo imekuwa ikidhamini. 
    Wachezaji wengi wazawa Afrika Kusini ambao wanawika katika klabu mbalimbali nchini humo na hata nje, wametokea kwenye mashindano hayo ya SAB.
    Kwa kugundua hilo, nikajiuliza inakuwaje kampuni hiyo wamilki wa TBL, wanaweza kuwekeza katika michezo ya vijana Afrika Kusini na si hapa Tanzania?
    Labda hawajaombwa na wahusika, yaani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Simba na Yanga. Labda.
    Tukumbuke, TBL walikuwa wadhamini wa michuano ya Kombe la Taifa, ambayo kwa sasa imekufa.
    Inaonekana kabisa kampuni hii ina sera nzuri za kusaidia michezo katika nchi ambazo wanafanya biashara, lakini kwa hapa Tanzania watu wameshindwa kutumia fursa.
    Je, katika dau la udhamini wa Simba, Yanga au Taifa Stars kuna bajeti maalum ya maendeleo ya vijana? Sijui- lakini wote Simba, Yanga na Taifa Stars wana timu vijana.
    Kama tunataka kuwa na timu imara za wakubwa za kushinda mataji, basi lazima tuwekeze katika soka ya vijana- je, TBL, Simba na Yanga katika mikataba yao wamezingatia hilo?
    Kama si hivyo, ni vyema basi TBL waipitie tena mikataba yao na Simba, Yanga na Taifa Stars na kufikiria namna ya kuweka mafungu kwa ajili ya maendeleo ya soka ya vijana.       Kila la heri. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA, YANGA NA TFF WAIPITIE UPYA MIKATABA YAO NA TBL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top