• HABARI MPYA

    Saturday, July 04, 2015

    KIPA WA CHELSEA AWASILI AZAM NA KUANZA MAZOEZI MOJA KWA MOJA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM 
    KIPA wa zamani wa mabingwa wa England, Chelsea FC, Vincent Atchouailou de Paul Angban amewasili jana usiku Dar es Salaam tayari kusaini Mkataba wa kujiunga na Azam FC. 
    Mlinda mlango huyo aliyezaliwa Februari 2, mwaka 1985 mjini Anyama, aliwasili pamoja na wachezaji wengine wawili wa Azam FC raia wa Ivory Coast, beki Serge Wawa Pascal na mshambuliaji KIpre Tchetche.
    Kipa huyo mrefu anayetokea klabu ya Ligi Kuu ya kwao, Ivory Coast, Jeunesse leo asubuhi alikuwepo mazoezini Azam FC katika ufukwe wa Cocoa Beach, Dar es Salaam.
    Vincent Angban aliwahi kuchezea timu ya vijana ya Chelsea chini ya umri wa mika 21 ingawa alikuwa amevuka umri huo katika harakati za kutafuta kusajiliwa The Blues, lakini pamoja na kuonyesha uwezo Stamford Bridge, haikuwa bahati yake jezi ya bluu.
    Vincent Angban (kulia) akiwa na kocha Muingereza wa Azam FC, Stewart Hall leo asubuhi Coco Beach

    Kipa huyo aliibukia katika klabu ya vijana ya Rio Sport d'Anyama kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza mwaka 2005, ambako hata hivyo miaka miwili baadaye aliondoka na kwenda kujiunga na Sawe Sports msimu wa 2006/2007.
    Mwaka 2007, Angban akajiunga na ASEC Mimosas ambako alikuwa kipa wa kwanza hadi mwanzoni mwa msimu wa 2009 alipoumia na nafasi yake kuchukuliwa na Daniel Yeboah. 
    Yeboah akawavutia zaidi makocha wa timu hiyo kwa ubora wake wa kuokoa michomo na akaendelea kudaka hata Angban alipopona.
    Baada ya kumaliza Mkataba wake ASEC, Angban akarejea Jeunesse na baadaye akaenda London kudakia U21 ya Chelsea.
    Amewahi kudakia timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Ivory Coast katika michuano ya Afrika nchini Benin mwaka 2005 na aliiwakilisha pia nchi yake katika Michezo ya Olimpiki mwaka 2008.
    Amedakia pia timu ya taifa ya wakubwa ya Ivory Coast ‘Tembo’ katika michuano ya CHAN ikiwemo ile ya mwaka 2009 na ndiye aliyesimama langoni katika mechi na Tanzania, Taifa Stars ikishinda 1-0 bao pekee la Mrisho Ngassa.   
    Azam FC inamchukua kipa huyo kwa lengo la kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya michuano ya Afrika- na kama inavyojulikana timu hiyo ya bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake mwakani itacheza Kombe la Shirikisho. 
    Akisani Azam FC, kipa huyo atakwenda kugombea namba na makipa wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Aishi Manula na Mwadini Ali.
    Kabla ya kuanza kwa ligi ya Bara hapo Agosti 22 mwaka huu, Azam pia imeshaanza maandalizi kwa ajili ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) ambayo yatafanyika nchini kuanzia wiki ijayo.
    Usajili wa kipa huyo ukikamilika, Azam itakuwa na wachezaji wanne kutoka Ivory Coast, wengine ni Serge Wawa Pascal na pacha, Kipre Herman Tcheche na Kipre Michael Balou.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPA WA CHELSEA AWASILI AZAM NA KUANZA MAZOEZI MOJA KWA MOJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top