• HABARI MPYA

  Tuesday, May 14, 2024

  KOMBE LA KAGAME KUFANYIKA TANZANIA JULAI


  TANZANIA imeteuliwa kuwa Mwenyeji wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame ambayo itafanyika kuanzia Julai 20 hadi Agosti 4.
  Taarifa ya Baraza la Vyama na Mashirikisho ya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) imesema Klabu zote bingwa za Ligi za ukanda huo unaohusisha mataifa 12 na nyingine nne zitakazoalikwa kutoka nje ya nchi wanachama zitashiriki.
  “Tunayo furaha kwamba michuano hii itarejea baada ya miaka miwili kuleta fursa nzuri ya maandalizi ya msimu kwa timu kujitayarisha vizuri kabla ya kuanza kwa msimu wa Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho ya CAF msimu wa 2024-2025 na Ligi tofauti za nyumbani,” amesema Mtendaji Mkuu wa CECAFA, John Auka Gacheo.
  Mara ya mwisho michuano hiyo ilifanyika Tanzania pia mwaka 2021 na Express ya Uganda ilitwaa Kombe kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya waalikwa, Nyasa Big Bullets Jijini Dar es Salaam.
  Simba SC ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo baada ya kushinda mara sita katika miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002 - sawa na Gor Mahia ya Kenya katika miaka ya 1967, 1979, 1982, 1983, 1984 na 1997.
  Vigogo wengine wa Tanzania, Yanga wanafuatia kubeba mara nyingi taji hilo, mara tano katika miaka ya 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012 sawa na Tusker, zamanı Breweries ya Kenya katika miaka ya 1988, 1989, 2000, 2001 na 2008.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOMBE LA KAGAME KUFANYIKA TANZANIA JULAI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top