• HABARI MPYA

  Thursday, May 16, 2024

  MAHODHA WA ZAMANI TAIFA STARS JELLAH MTAGWA AFARIKI DUNIA


  BEKİ na Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars Jellah Mtagwa (71) amefariki dunia leo katika Hospitali ya Muhimbili Mloganzila alipokuwa amelazwa kwa matibabu.
  Mtagwa aliyekuwa beki hodari wa kati enzi zake - amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya Kiharusi tangu mwaka 2004 kufuatia kuanguka akiwa anatembea katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
  Mtagwa alikuwa Nahodha wa Taifa Stars kwa miaka 10 mfululizo kuanzia mwaka 1973 akimrithi beki wa kati pia, Omar Zimbwe hadi 1983 alipomuachia Charles Boniface Mkwasa mlinzi pia na kiungo.
  Aliiongoza Taifa Stars kufuzu Fainali za Kwanza za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria na mwaka 1982 sura yake iliwekwa kwenye stempu kutokakana na umaarufu wakati huo.
  Ilikuwa wakati wa mechi za Kufuzu Kombe la Dunia mwaka 1982 nchini Hispania ambazo Taifa Stars ilitolewa na Nigeria katika Raundi ya Pili baada ya kuitoa, Kenya katika Raundi ya kwanza ya mchujo huo.
  Jellah alizaliwa mwaka 1953 Morogoro mjini akapata elimu ya msingi shule ya Mwembesongo na baadaye kujiunga na Sekondari ya Morogoro (Moro Sec) na kumaliza mwaka 1975.
  Kisoka aliibukia Nyota Afrika ya Morogoro, kabla ya kusajiliwa Yanga mwaka 1974 akiwa Kidato cha Nne na ambako alicheza kwa misimu miwili na miezi kadhaa hadi mwaka 1976.
  Aliondoka kufuatia mgogoro mkubwa wa kihistoria uliotokea Yanga mwaka 1976 na Kundi kubwa la wachezaji likamfuta Mwenyekiti aliyefukuzwa na wanachama, Tarbu Mangala na Meneja Shiraz Sharrif kwenda kuasisi klabu ya Pan Africans.
  Alicheza Pan Africans hadi mwaka 1984 alipolazimika kustaafu kufuatia kuumia goti la mguu wa kushoto akiichezea Taifa Stars baada ya kugongana na mshambuliaji wa Zambia, Michael Chabala - licha ya kufanyiwa upasuaji na Daktari bingwa wa mifupa, Dk Philemon Sarungi, aliyewahi kuwa Daktari wa Taifa Stars na Waziri wa Michezo, lakini hakuweza kurudi dimbani.
  Msiba upo nyumbani kwake, eneo la Friends Corner, Manzese Jijini Dar es Salaam na taratibu za mazishi zitatolewa.
  Ameacha mke na watoto watano pamoja na wajukuu kadhaa.
  Mungu ampumzishe kwa amani Jellah Mtagwa. Amin. 


  Jellah Mtagwa (wa pili kutoka kulia waliosimama katika Taifa Stars mwaka 1982.
  Wengine kulia ni Salim Amir, anayefuatia baada ya Jellah Mtagwa ni Athumani Mambosasa (sasa marehemu), Juma Mkambi ‘Jenerali’ (sasa marehemu), Mohamed Salim, Augustino Peter ‘Tino’ na kocha, Joel Bendera (sasa marehemu). Waliochuchumaa kutoka kulia ni Daudi Salum ‘Bruce Lee’, Omar Hussein ‘Keegan’, Mohammed ‘Adolph’ Rishard, Hussein Ngulungu na Mohamed Kajole (sasa marehemu).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAHODHA WA ZAMANI TAIFA STARS JELLAH MTAGWA AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top