• HABARI MPYA

    Wednesday, July 01, 2015

    KAMA TUKO TAYARI KUFA, SASA TUNAITAFUTA PEPO!

    JAMBO moja niliamua kufanya mwishoni mwa wiki ni kusafiri hadi Mbeya kwenda kuiona timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 15 ikicheza mechi za kujipima nguvu.
    Vijana hao walio chini ya kocha Bakari Shime wanaandaliwa kwa ajili ya kucheza mechi za kufuzu Fainali za Vijana Afrika chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2017 na kila wiki ya mwisho wa mwezi watakuwa wakikutana kwa mazoezi na michezo ya kujipima nguvu.
    Kwa sababu wote ni wanafunzi katika shule mbalimbali nchini, wametengenezewa programu maalumu na kila wanapofunga shule wanakuwa na kambi ndefu na ziara za nje ya nchi kujipima zaidi.
    Mchezo wa kwanza Jumapili walishinda mabao 3-0 dhidi ya Kombaini y vijana chini ya umri wa 17 ya Mbeya Uwanja wa Sokoine mjini humo.
    Katika mchezo huo uliohudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi dakika 45 za kwanza zilimalizika U15 wakiwa mbele kwa bao 1-0.
    Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji Timoth Maziku dakika ya 17 kwa guu la kulia akimalizia krosi ya Nahodha Issa Abdi.
    Baada ya bao hilo, Mbeya Kombaini walitulia na kuanza kusukuma mashambulizi langoni mwa timu ya taifa, hali ambayo ilifanya timu hizo zishambuliane kwa zamu huku pia vijana wakionyesha uwezo wa kuridhisha.
    Dakika ya 72, Albinius Haule almanusra aisawazishie bao Mbeya kama si shuti lake zuri la kitaalamu alilopiga kutoka umbali wa mita 25 kugonga mwamba wa juu na kutoka nje.
    Nahodha Issa Abdi aliifungia timu ya taifa bao la pili dakika ya 82 kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya Timoth Maziku kuangushwa nje kidogo ya boksi na Richard Paul.
    Emmanuel Ntindi wa Mbeya alijifunga dakika ya 87 katika harakati za kuokoa krosi ya Asad Ally dhidi ya Maziku.
    Mchezo ulikuwa mzuri, vijana walionyesha ufundi wa hali ya juu- na Mbeya pamoja na kufungwa, ilicheza vizuri na kilichowakwamisha kupata japo bao moja ni uhodari wa kipa Kelvin Deogratius wa U15 ya taifa.
    Mchezo wa marudiano Jumatatu jioni wakashinda 4-1 na jana jioni timu imerejea Dar es Salaam na vijana kuvunja kambi hadi watakapokusanywa tena mwishoni mwa mwezi huu kwa safari ya Zanzibar kwa michezo mingine ya kujipima.
    Mkakati wa TFF ni hivi karibuni kuliongezea nguvu benchi la Ufundi kwa kuleta mwalimu wa kigeni atakayefanya kazi pamoja na Shime- lakini pia ni kuwa na programu endelevu ya kuwaandaa vijana hao kabla ya kuanza mechi za kufuzu fainali za U17 2017 mwakani.
    Tanzania imepewa uenyeji wa fainali za U17 mwaka 2019 na tayari kuna vijana wengine chini ya umri wa miaka 13 wamekwishakusanywa wanaandaliwa kwa ajili ya michezo hiyo.
    Wakati huo huo, U17 hii ndiyo itakuwa U20 ambayo mkakati ni icheze hadi Fainali za Dunia, ndiyo itakuwa U23 ambayo mkakati ni icheze hadi Olimpiki ya 2020 mjini Tokyo, Japan.
    TFF inataka vijana hawa waipeleke Tanzania AFCON ya 2021 nchini Ivory Coast na Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.
    Na wakati hawa wanacheza kupanda hadi Kombe la Dunia, nyuma yao tayari kuna vijana watakuwa wanafuata nyayo zao, watawarithi kila watakapoinua mguu yao.
    Mpango mkakati wa TFF unaonyesha kwamba, utaratibu huo utaendelea kuhakikisha wakati wote tunakuwa na timu imara ya taifa kuanzia daraja la mwisho la timu ya vijana.
    Siku zote tumekuwa tukipigia kelele juu ya kuwekeza kwenye soka ya vijana ili kuhakikisha tunakuwa na timu bora za taifa wakati wote.
    Klabu zimeshindwa kutusaidia katika dhana ya uwekezaji kwenye soka ya vijana na wameona bora tuwe na Ligi Kuu kama ya England yenye wachezaji wengi wa kigeni- sasa ni saba maana ni zaidi ya Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini.
    Mpango huu wa soka ya vijana TFF inapaswa kuuwekea umakini wa hali ya juu kupita inavyofikiria- ili kuhakikisha tunandaa vijana watakaokuwa wachezaji kweli tofauti na hawa wa sasa ambao wengi wao ni ‘mabange’ tu.
    Kuhakikisha kijana siyo tu anaandaliwa kuwa timamu kiuchezaji, bali hata kimaadili pia. Tumemsikia Rais wa TFF, Jamal Malinzi akisema U15 ya sasa baadaye itakwenda hadi nje ya nchi kucheza na U17 za huko kabla ya kuanza mechi za kuwania fainali za U17 ya 2017.
    Huu ni mkakati uliobeba matumaini ya soka ya Tanzania na kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya nchi, hatimaye tuna Mpango Mkakati thabiti wa soka ambao umekwishaanza kufanyiwa kazi.
    Wito wangu kwa wadau, Serikali na makampuni, wausapoti mradi huu. Mradi huu ndiyo utakaoijengea heshima soka ya Tanzania bila shaka kwa maana zote, kuwa na timu bora za taifa ambazo kuanzia mwaka 2020 zitakuwa hazikosi fainali za mashindano makubwa na pia kuwa na wachezaji wakubwa wanaocheza Ulaya. 
    Siku zote Watanzania tumekua tukitaka kwenda peponi bila ya kufa- matokeo yake tumekuwa tukivurugana wenyewe hapa na kushikana uchawi. 
    Sasa wote tuimbe wimbo mmoja, tuna programu ya mpito ndiyo hii ya Charles Boniface Mkwasa, tutaendelea nayo na tutacheza mechi za kufuzu michuano yote. Tukitolewa huku, tutahamia kule. 
    Lakini mpira rasmi tutarajie kuanza kuucheza kuanzia mwaka 2020. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMA TUKO TAYARI KUFA, SASA TUNAITAFUTA PEPO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top