• HABARI MPYA

    Monday, June 15, 2015

    UKISHANGAA “MAPENZI HAYANA DHAMANA” YA ISHA MASHAUZI, UTASTAAJABU NA “WALE WALE” YA VIJANA NGWASUMA

    TUZO kubwa za muziki hapa nchini - Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) 2015 zilitolewa Jumamosi iliyopita kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam ambapo kama ilivyo kawaida ya miaka yote, malalamiko hayakukosekana.
    Ali Kiba akaibuka kidedea na kumtupa vibaya mpinzani wake mkubwa Diamond Platnumz - Baadhi ya watu wananong’ona eti Kiba kabebwa, kwamba kuna njama za makusudi za kumshusha Diamond.
    Kiba amechukua tuzo tano ikiwemo ya mwimbaji bora wa kiume wa mwaka na ile ya mtumbuizaji bora wa kiume wa mwaka, wakati Diamond ameambulia tuzo mbili tu. Swahiba wangu Christian Bella ambaye kwangu mimi nasema alipangwa kwenye makundi ya “kifo” ametoka mtupu kwa kushindwa kuambulia tuzo hata moja.
    Kibinaadamu yako mapungufu yanayoweza kujitokeza kila mwaka na hii ipo katika kila  nyanja, si muziki tu – haitatokea hata mwaka mmoja tuzo zikakosa malalamiko, labda kama zitahamishiwa kwenye sayari nyingine. Bendi, msanii au mshabiki ukishaamini kuwa kuna kubebana, basi wewe tayari umefeli kwa kuwa akili yako imeshadumaa na kuamini katika kushindwa.
    Hizi ni tuzo za wananchi, mtaji mkubwa wa tuzo hizi ni kura za wananchi, ukiwa huna mashabiki wengi wa kukupigia kura ujue imekula kwako. Kama unakaa mitandaoni au vijiweni na kupoteza muda mwingi kwa kukandia kazi za wasanii wengine badala ya kutumia muda huo kunadi kazi zako au zile unazozishabikia, basi wewe utakuwa na matatizo ya akili na mwisho wa siku wakati wenzako wananyanyua juu tuzo zao, wewe utakuwa unawaza namna ya kuja na hoja mpya juu ya sera zako za kubebana. Pole yako.
    Hizi sio tuzo za kisiasa, si tuzo za huruma – kwamba mwaka jana fulani alikosa basi mwaka huu apewe, au fulani ana tuzo tano basi moja tuipunguze iende kwa yule ili kila mtu aambulie japo kiduchu, hakunaga kitu kama hicho.
    Ongeza ubunifu kwenye kazi zako ili ujiongezee mashabiki wa kazi zako ambao mwisho wa siku ndio wanakuwa mtaji wako wa kuelekea kunyakua tuzo.
    Kuna wimbo “Mapenzi Hayana Dhamana” wa Isha Mashauzi ambao umeshinda  tuzo ya wimbo bora wa taarab, baadhi ya watu wamekuwa wakilalamika kuwa huu sio wimbo wa taarab, watu wao wakatumia nguvu kubwa mitandaoni kuupiga vita huku wakisahau kuhamasisha kazi wanazozishabikia.
    Lakini kwa upande wa pili, mashabiki wa Isha badala ya kupoteza muda kubishana na watu hao, wao wakaongeza nguvu ya kuhamasishana kupiga kura, walijua wazi kuwa mtaji wa tuzo ni kura na si majungu.
    Mapenzi Hayana Dhamana ni wimbo mzuri uliojaa mageuzi yanayohitajika hasa katika kipindi hiki ambacho nyimbo kibao za taarab zimekuwa zikirekodiwa kila kukicha na kufanya nyimbo nyingi zifanane na hivyo kuanza kuporomosha soko la muziki huu wa mwambao.
    Alichofanya Isha ni kulisoma soko na kisha kujitofautisha na kujitengenezea utambulisho (identity) wa kipeke yake kitu ambacho mwisho wa siku kimezaa matunda.
    Lakini pia kuna wimbo “Wale Wale” wa Vijana Ngwasuma ambao umechukua tuzo ya wimbo bora wa bendi za dansi. Wako wanaosema ule si wimbo wa dansi.
    Kwangu mimi nasema “Wale Wale” ni aina nyingine ya ubunifu uliotukuka – wimbo mzuri, mfupi na umejitofautisha na nyimbo nyingi za dansi tulizozizoea.
    Umeshawi kukutana na wimbo unaisha halafu unanuna au kulaani kwanini umeishia hapo? “Wale Wale” ni moja ya nyimbo za aina hiyo.
    Soko la taarab na dansi linavamiwa kwa nguvu na muziki wa bongo fleva, bila kuongeza ubunifu basi anguko kubwa la kibiashara litawakuta. Kama tunasema siku hazigandi basi kwanini na nyinyi msiseme soko haligandi? ‘big up Mapenzi Hayana Dhamana, big up “Wale Wale”. Wanaowashangaa waambieni wasisahau kustaajabu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UKISHANGAA “MAPENZI HAYANA DHAMANA” YA ISHA MASHAUZI, UTASTAAJABU NA “WALE WALE” YA VIJANA NGWASUMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top