• HABARI MPYA

  Monday, December 01, 2014

  ‘MIDO’ LA GAMBIA LAANZA KAZI SIMBA SC

  na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  KIUNGO mshambuliaji wa Gambia, Omar Mboob ameanza majaribio leo katika klabu ya Simba SC, baada tu ya kuwasili nchini.
  Simba SC imefanya mazoezi leo asubuhi, ikianzia Gym na baadaye Uwanja wa Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam na Mgambi huyo  alishiriki kikamilifu.
  Makamu wa Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema kwamba Mboob, anayetokea klabu ya Samger ya Gambia atakuwa majaribioni kwa wiki mbili.
  Simba SC inajaribu kutaka kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kushinda mechi moja tu kati ya saba, nyingine zote ikitoa sare.
  Omar Mboob akipokea maelekezo kutoka kwa Kocha Msaidizi wa Simba SC, SUleiman Matola leo asubuhi mazoeizni
  Omar Mboob akiwa mazoezini Gym eneo la Chang'ombe mjini Dar es Salaam na SImba SC

  Hata hivyo, Simba SC ikivutiwa na Mboob italazimika kukata mchezaji mmoja wa kigeni ili imajili, kwa kua tayari kwa sasa inao watano.
  Wakati Mganda Dan Sserunkuma tayari anatarajiwa kuchukua nafasi ya majeruhi Mkenya, Paul Kiongera, Simba SC inao pia Waganda Joseph Owino, Emmanuel Okwi na Warundi Pierre Kwizera na Amisi Tambwe. 
  Kiongera anaondoka kesho Dar es Salaam kwenda India kwa matibabu, lakini klabu yake Simba SC imemuondoa kwenye orodha ya wachezaji watakaocheza sehemu iliyobaki ya Ligi Kuu.
  Mfungaji bora wa Kenya kwa misimu miwili iliyopita, Daniel Sserunkuma atarejea Dar es Salaam Jumatano kusaini Mkataba wa mwaka mmoja baada ya mazungumzo yaliyopata mwafaka wiki iliyopita.
  Na mshambuliaji huyo wa Gor Mahia ya Kenya ndiye atakayechukua nafasi ya Mkenya, Kiongera ambao waliwahi kucheza pamoja klabu hiyo ya Nairobi chini ya kocha Mcroatia, Zdravko Logarusic.
  Kwa kuwa baada ya kufanyiwa upasuaji India, Kiongera atahitaji si chini ya miezi mitatu ya mapumziko, maana yake atarejea Ligi Kuu ikiwa imefika ukingoni, Simba SC imeona bora imuondoe katika usajili.
  Lakini Simba SC haina kabisa mpango wa kumtema Kiongera, zaidi ya kumtibu apone ili baadaye aje kuitumikia klabu- isipokuwa Mkataba wake utasogezwa mbele kwa maana ya kipindi cha matibabu kutohesabiwa kama alikuwa kazini.
  Simba SC ilimsajili Kiongera akiwa majeruhi kutoka Kenya na kwa bahati mbaya akatonesha goti lake katika mchezo wa kwanza tu wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union. Awali, mchezaji huyo mrefu alicheza mechi tatu za kirafiki na kufunga mabao mawili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ‘MIDO’ LA GAMBIA LAANZA KAZI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top