• HABARI MPYA

    Sunday, November 16, 2014

    KIMENUKA MBEYA CITY, KOCHA MWAMBUSI ABWAGA MANYANGA ‘KIMYA KIMYA’ NA SIMU ZOTE KAMPA MKEWE APOKEE

    Na Mwandishi Wetu, MBEYA
    HAMKANI si shwari Mbeya City, baada ya kuwapo kwa taarifa kocha Juma Mwambusi ameacha kazi.
    Hatua hiyo inakuja baada ya Mbeya City kushinda mechi moja kati ya saba za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara hadi sasa, mbili nyingine ikitoa sare na nne kufungwa hivyo kuambulia pointi tano na kujikuta inashika mkia.
    Mwalimu Mwambusi hakupokea simu yake mara mbili alipotafutwa na BIN ZUBEIRY. Mara zote alipokea mke wake na kusema kwamba mumewe amekwenda hospitali na ameacha simu zake zote nyumbani.
    Mwambusi ameacha kazi Mbeya City

    Mama Mbwambusi alipoulizwa inakuwaje mumewe aondoke bila simu zake zote, akasema; “Amekurupushwa tu asubuhi asubuhi, amekwenda hospitali kaacha simu zote hapa,”.
    Na alipoulizwa kama ana taarifa za mumewe kuacha Mbeya City, akasema; “Mimi sijui lolote,”.
    Mwambusi ndiye aliyeipandisha Mbeya City Ligi Kuu msimu uliopita na moja kwa moja ikaanza kwa kishindo ikimaliza katika nafasi ya tatu, mbele ya mabingwa wa zamani, Simba SC.
    Hata hivyo, pamoja na mafanikio ya msimu uliopita, kibao kimegeuka msimu huu na timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya imepoteza makali yake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIMENUKA MBEYA CITY, KOCHA MWAMBUSI ABWAGA MANYANGA ‘KIMYA KIMYA’ NA SIMU ZOTE KAMPA MKEWE APOKEE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top