• HABARI MPYA

    Wednesday, July 16, 2014

    MWINYI KAZIMOTO ATUA KESHO DAR STARS IKIREJEA KUTOKA TUKUYU, SAMATTA, ULIMWENGU WAANZA MAZOEZI KIVYAO LEO

    Na Boniface Wambura, DAR ES SALAAM
    KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Mwinyi Kazimoto anatarajiwa kuwasili kesho Saa 1:30 asubuhi kwa ndege ya Qatar Airways, akitokea Qatar anakocheza soka ya kulipwa.
    Mchezaji huyo wa zamani wa Simba SC na JKT Ruvu, kwa sasa anacheza klabu ya Al Markhiya ya Qatar na anakuja nchini kujiunga na kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Msumbiji Jumapili wiki hii.
    Tayari wachezaji wengine wa nje, washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamewasili nchini leo asubuhi.
    Mwinyi Kazimoto atawasili kesho Dar es Salaam

    Samatta na Ulimwengu wameasili wakitokea Tunisia ambako Mazembe imeweka kambi ya kujiandaa na mechi za Kundi lake, A Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Taifa Stars itamenyana na Msumbiji ‘Mambas’ Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho ya mchujo, kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco.
    Wachezaji hao wamefikia hoteli ya Courtyard, iliyopo eneo la Sea View, Upanga mjini Dar es Salaam na leo  watafanya mazoezi kwa programu maalumu waliyopewa na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij wakati wakiwasubiri wenzao watakaowasili kesho kutokea Tukuyu, Mbeya walipoweka kambi.
    Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itawasili Dar es Salaam kesho Saa 3:20 asubuhi kwa ndege ya Fastjet kutoka Mbeya tayari kwa maandalizi ya mwisho kabla ya kuivaa Msumbiji.
    Katika hatua nyingine, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atakuwa na mkutano na waandishi wa habari keshokutwa kuanzia Saa 5:00 asubuhi kwenye ofisi mpya za shirikisho hilo, katikati ya Jiji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWINYI KAZIMOTO ATUA KESHO DAR STARS IKIREJEA KUTOKA TUKUYU, SAMATTA, ULIMWENGU WAANZA MAZOEZI KIVYAO LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top