• HABARI MPYA

  Friday, October 12, 2018

  MKUU WA MKOA MTWARA AWAONDOA VIONGOZI NDANDA FC, AUNDA KAMATI YA WATU 10 KUSIMAMIA TIMU

  Na Mwandishi Wetu, MTWARA
  MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Gilasius Byakanwa amefanya mabadiliko katika uongozi wa klabu ya Ndanda FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Mtwara, Byakanwa amesema kwamba amechukua hatua hiyo akiwa kama mlezi wa timu kwa kuuweka pembeni uongozi wa uliokuwepo madarakani  kutokana na kushindwa kuiendesha timu hadi imegeuoka ombaomba wa kudumu. 
  Mkuu huyo wa Mkoa ameunda Kamati maalum ya watu 10 itakayosimamia timu hiyo kwa kipindi cha msimu wa ligi kilichosalia ambayo itaongozwa na Laurent Paul Werema, atakayeshirikiana na Stanley Milanzi, Athumani Kambi, Raymond Kasuga, Joseph Peneza, Baldwin Massawe, Mohammed ‘Mamu’ Remtullah, Mohammed Nassor, Kotensi Luiza, Khalid Said Mkwila na Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’.

  Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gilasius Byakanwa amefanya mabadiliko katika uongozi wa klabu ya Ndanda FC 

  “Tutakubaliana na wapenzi wa michezo na wadau wa michezo kwamba, kuendesha timu kunahitaji gharama za fedha. Sasa huwezi kuwa na viongozi ambao wakikutana hawawezi hata kununua maji kwa ajili ya wachezaji, au huwezi kuwa na viongozi wa timu, ambao wakikutana wanafikiria kile kilichoingia kwenye timu ndicho kiwasaidie wao wenyewe kwa matumizi yao binafsi,”amesema Byakanwa.   
  Hatua ya Mkuu huyo wa mkoa inakuja baada ya Ndanda FC kuzuiliwa mkoani Mtwara kwa deni la Sh. Milioni 3.5 hadi ilipokwamuliwa na msanii wa Bongo Fleva, Rajab Abdul Kahali, maarufu kama Harmonize. 
  Ndanda FC walizuiwa kuondoka hotelini mjini Singida baada ya mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Singida United wakifungwa 3-1 Oktoba 6 Uwanja wa Namfua kwa deni la Sh. Milioni 3.5.
  Uongozi wa Ndanda FC ulitoa taarifa ya kuomba misaada kwa wadau mbalimbali wa soka wa mkoani Mtwara kuichangia timu hiyo iweze kulipa deni na kuruhusiwa kuondoka, lakini bahati nzuri iliyoje, Harmonize pekee amemaliza tatizo.
  Na uongozi wa Ndanda FC ulimshukuru mwanamuziki huyo msaliwa wa Mtwara,anayemilikiwa na lebo ya WCB Wasafi Record, iliyo chini ya msanii nyota wa Bongo Fleva, Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’.
  Harmonize anayefahamika zaidi kwa wimbo wake Bado aliomshirikisha bosi wake, Diamond Platnumz amekuwa akihudhuria mechi za Ndanda na kujitambulisha kama shabiki wa timu hiyo ya nyumbani kwao.
  Ndanda FC inashika nafasi ya 15 katika Ligi Kuu ya timu 20, ikiwa imejikusanyia pointi nane katika mechi nane na kwa ujumla msimu huu unatarajiwa kuwa mgumu kwa timu nyingi kifedha kutokana na waliokuwa wadhamini wakuu wa ligi, Vodacom kujitoa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MKUU WA MKOA MTWARA AWAONDOA VIONGOZI NDANDA FC, AUNDA KAMATI YA WATU 10 KUSIMAMIA TIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top