• HABARI MPYA

    Friday, October 05, 2018

    LIPULI FC WANUSURIKA KUPIGWA NYUMBANI NA STAND UNITED, WASAWAZISHA ‘JIONI’ KUPATA SARE 1-1 SAMORA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Lipuli FC  jioni ya leo imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Samora mjini Iringa.
    Na haikuwa kazi nyepesi hata kupata sare hiyo ya nyumbani, kwani Lipuli ya kocha Suleiman Matola ililazimika kusubiri hadi dakika 20 za mwisho ili kusawazisha.
    Hiyo ni baada ya Stand United kutangulia kwa bao la Sixtus Sabilo dakika ya 48, kabla ya Issa Rashid kuisawazishia Lipuli FC dakika ya 79.
    Kwa sare hiyo, kila timu inajiongezea pointi moja, Lipuli FC wakifikisha pointi nane baada ya kucheza mechi nane na Stand United wakifikisha pointi 11 katika mechi ya tisa.
    Lipuli FC leo imelazimishwa sare ya 1-1 na Stand United Uwanja wa Samora 

    Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea kesho kwa mechi tano; Uwanja wa Namfua mjini Singida, wenyeji Singida United watawakaribisha Ndanda FC, Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na wenyeji Simba SC watamenyana na African Lyon.
    Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Sugar watawakaribisha Ruvu Shooting, Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya kutakuwa na mechi ya mahasimu wa Jiji la Mbeya, Tanzania Prisons na Mbeya City wakati Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar watamenyana na KMC.
    Jumapili kutakuwa na mechi nyingine tatu, Yanga SC wakimenyana na Mbao FC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Uwanja wa Meja Isamuhyo huko Mbweni, JKT Tanzania watamenyana na Alliance FC na Uwanja wa Karume mjini Musoma, Biashara United watakuwa wenyeji wa Mwadui FC, wakati JUmatatu Azam FC watawakaribisha Coastal Union.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LIPULI FC WANUSURIKA KUPIGWA NYUMBANI NA STAND UNITED, WASAWAZISHA ‘JIONI’ KUPATA SARE 1-1 SAMORA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top