• HABARI MPYA

    Monday, September 11, 2017

    LWANDAMINA: TUMESHINDA LAKINI TULICHEZA KATIKA MAZINGIRA MAGUMU

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mzambia wa Yanga, George Lwandamina amesema kwamba timu yake ilishinda kucheza vizuri jana dhidi ya wenyeji, Njombe Mji kwa sababu Uwanja mbaya na hali ya hewa ya baridi kali.
    Yanga SC jana wamevuna pointi tatu za kwanza katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji, Njombe Mji Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe.
    Shukurani kwake, mshambuliaji mpya, Ibrahim Hajib Migomba aliyefunga bao hilo pekee kipindi cha kwanza na sasa Yanga inafikisha pointi nne baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Lipuli ya Iringa kwenye mchezo wa kwanza nyumbani, Dar es Salaam. 
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Suleiman Kinugani wa Morogoro, aliyesaidiwa na Khalfan Sika wa Pwani na Hajji Mwalukuta wa Tanga, Hajib alifunga bao hilo dakika ya 16 kwa shuti la umbali wa mita 30 la mpira wa adhabu, baada ya yeye mwenyewe kuangushwa.
    Kocha wa Yanga, George Lwandamina amesema timu yake haikucheza vizuri jana Njombe kwa sababu Uwanja mbaya na baridi kali

    Na baada ya mchezo huo, Lwandamina leo amesema kwamba hawakucheza katika kiwango chao kutokana na mazingira ya Uwanja na hali ya hewa, lakini wanashukuru wamechukua pointi tatu.
    “Ninamshukuru Mungu tumeshinda, lakini ulikuwa mchezo mgumu sana kutokana na mazingira magumu ya Uwanja wa na hali ya hewa,”alisema.
    Kocha wa zamani wa Zesco United ya kwao, Zambia amesema kwamba sasa anaelekeza nguvu kwenye mchezo ujao dhidi ya Maji Maji ya Songea, ambao pia anatarajia utakuwa mgumu kwa sababu atakuwa anacheza kwenye mazingira ya aina sawa na Njombe.
    Yanga watakuwa wageni wa Maji Maji Jumamosi wiki hii Uwanja wa Maji Maji mjini katika mchezo wa tatu wa Ligi Kuu na wa pili mfululizo ugenini baada ya kuvuna pointi nne katika mechi zilizotangulia kufuatia sare ya 1-1 na Lipuli Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na ushindi wa jana. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LWANDAMINA: TUMESHINDA LAKINI TULICHEZA KATIKA MAZINGIRA MAGUMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top