• HABARI MPYA

  Monday, April 10, 2023

  BALEKE ‘MTU MBAYA’ AIMALIZA IHEFU DAKIKA ZA MWISHONI MBARALI


  MSHAMBULIAJI Mkongo, Jean Toria Baleke Othos ametumia dakika nane za mwisho kuifungia Simba SC mabao yote ikiibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Ihefu SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Highland Estate, Ubaruku, Mbarali mkoani Mbeya.
  Baleke ambaye Aprili 17 atafikisha umri wa miaka 22 tu, alifunga dakika ya 84 akimalizia pasi ya kiungo Msenegal, Pape Ousmane Sakho na dakika ya 87 akimalizia mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kufuatia yeye mwenyewe kuunganisha kwa kichwa krosi ya Kibu Dennis.
  Simba SC inafikisha pointi 60 katika mchezo wa 25 ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa pointi tano na mabingwa watetezi, Yanga ambao pia wana mechi moja mkononi na kesho wanacheza na Kagera Sugar Dar es Salaam.
  Ihefu SC wanabaki na pointi 33 za mechi 26 nafasi ya saba a baada ya kupoteza mechi ya pili mfululizo mbele ya Simba ndani ya siku ya nne kufuatia kichapo cha 5-1 kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) Ijumaa Jijini Dar es Salaam.
  Mapema kabla ya mchezo huo kuanza Baleke aliyefunga mabao matatu kwenye mechi ya ASFC dhidi ya Ihefu Ijumaa, alikabidhiwa tuzo yake ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu mwezi Machi, huku kocha wake, Mbrazil Robert Oliveira ‘Robertinho’ akipewa ya Kocha Bora.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BALEKE ‘MTU MBAYA’ AIMALIZA IHEFU DAKIKA ZA MWISHONI MBARALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top