• HABARI MPYA

  Sunday, December 19, 2021

  YANGA YAZIMA GWARIDE SUMBAWANGA, PRISONS CHALI


  VIGOGO, Yanga SC wametoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya wenyeji, Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.
  Tanzania Prisons iliyokuwa inaongozwa na Kocha Msaidizi na mchezaji wa zamani wa timu hiyo ilitangulia kwa bao la Samson Mbangula kwa kichwa dakika ya 12 akimalizia mpira wa Kona wa Lambert Sabiyanka kutoka upande wa kushoto.
  Kiungo Mzanzibari, Feisal Salum ‘Fei Toto’ akaisawazishia Yanga dakika ya 23 kwa shuti kali baada ya kazi nzuri ya kiungo Mganda, Khalid Aucho ambaye yeye mwenyewe alifunga bao Lila ushindi dakika ya 43 kwa kichwa cha kuchupia mpira chini chini kufuatia krosi ya kiungo Mrundi, Said Ntibazonkiza.


  Kwa ushindi huo, Yanga SC inayofundishwa na kocha Mtunisia, Nasreddine Nabi akisaidiwa na Mrundi, Cedric Kaze inafikisha pointi 23 baada ya kucheza mechi tisa sasa na kuendelea kuongoza ligi kwa pointi tano zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao wamecheza mechi nane.
  Hali ni mbaya kwa Tanzania Prisons inayobaki na pointi zake nane za mechi tisa katika nafasi ya 13 kwenye ligi ya timu 16, ambayo mwisho wa msimu mbili zitashuka na mbili zitakwenda kucheza na timu za Championship kuwania kusalia Ligi Kuu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YAZIMA GWARIDE SUMBAWANGA, PRISONS CHALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top