• HABARI MPYA

    Friday, December 10, 2021

    TFF YASEMA BARUA YA CAF KUIZUIA GSM NI FEKI


    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema kwamba barua inayosambaa mitandaoni ikidaiwa imetoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kusitisha udhamini wa GSM katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara ni ya kufoji.
    Jioni ya leo ilisambaa barua mitandaoni ikionyesha imetoka CAF ikiiagiza TFF kutoweka mabango ya wadhamini wapya wa Ligi Kuu, kampuni ya GSM katika mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga kesho Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
    Barua hiyo ilisema hatua hiyo ni kufuatia malalamiko kutoka klabu ya Simba juu ya udhamini wa GSM, ambao pia ni wadhamini wa wapinzani wao, Yanga.


    Awali, Simba iliiandikia barua Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TPLB) kuhoji juu ya mkataba wa udhamini wa kampuni ya GSM katika Ligi Kuu huku pia wakiwa wadhamini wa wapinzani wao, Yanga SC.
    Katika barua hiyo iliyosainiwa na Mtendaji Mkuu wa Simba, klabu hiyo, Barbara Gonzalez ilisema haifahamu kwa undani juu ya mkataba huo wao watanufaika vipi zaidi tu ya kufahamishwa kutumia nembo ya GSM kwenye tiketi na jezi zao wakati wa mechi za ligi hiyo.
    Lakini pia Simba ilisema GSM kuwa wadhamini wa Ligi Kuu wazi inaleta mgongano wa kimslahi kwa sababu ni wadhamini wa Yanga pia, klabu ambayo kwa pamoja na mdhamini wao lengo lao ni kutwaa ubingiwa ligi kama wao.


    Novemba 23, mwaka huu GSM iliingia mkataba wa Udhamini Mwenza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa dau la Sh. Bilioni 2.1 kwa miaka miwili.
    Na barua iliyodaiwa kutoka CAF leo imeagiza matumizi yote ya nembo za mdhamini huyo mpya yasitishwe hadi hapo itakapoifanyia kazi kesi hiyo na kutoa uamuzi.
    Mapema leo, kocha wa Simba, Mspaniola Pablo Franco Martin aligoma kushiriki mkutano na Waandishi wa Habari kuelekea mchezo wa kesho kwa sababu ya kuwepo mabango ya GSM nyuma ya meza.



    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YASEMA BARUA YA CAF KUIZUIA GSM NI FEKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top