• HABARI MPYA

  Jumatano, Septemba 04, 2019

  YANGA SC WAENDA MWANZA KUWEKA KAMBI YA KUJIANDAA NA MCHEZO DHIDI YA ZESCO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha Yanga SC kimeondoka leo mjini Dar es Salaam kwenda mjini Mwanza kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wake ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United ya Zambia.
  Yanga SC watakuwa wenyeji wa Zesco United Septemba 14 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Na katika kujiandaa na mchezo huo, kikosi kimeondoka leo kwenda Mwanza kuweka kambi na kikiwa huko kitapata pia mechi mbili za kujipima nguvu.

  Mchezo wa kwanza Yanga SC itacheza dhidi ya Gwambina FC ya Misungwi Jumamosi kabla ya kumenyana na Toto Africans ya Mwanza, michezo ambayo yote itaonyeshwa na Azam TV.
  Kabla ya kwenda kurudiana na Zesco United Septemba 27 mwaka huu mjini Ndola nchini Zambia, Yanga SC watakuwa na mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City Septemba 18 Uwanja wa Sokoine.
  Yanga SC ilifanikiwa kuingia hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa baada ya kuitoa Towsnhipa Rollers ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1, ikianza na sare ya 1-1 nyumbani kabla ya kwenda kushinda 1-0 Gaborone.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WAENDA MWANZA KUWEKA KAMBI YA KUJIANDAA NA MCHEZO DHIDI YA ZESCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top