• HABARI MPYA

  Monday, October 02, 2017

  TANZANIA YATANDIKWA 6-0 NA NIGERIA KUFUZU KOMBE LA DUNIA

  Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
  TIMU ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 nchini, Tanzanite imetupwa nje ya michuano ya kuwania kucheza fainali za Dunia mwakani Ufaransa, baada ya kukubali kichapo cha mabao 6-0 kutoka kwa Nigeria katika mechi iliyopigwa Jumapili kwenye uwanja wa Azam Complex,  Chamazi. 
  Tanzanite imetolewa kwenye michuano hiyo kwa jumla ya mabao 9-0, baada ya awali kufungwa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza nchini Nigeria. 
  Katika mechi ya marudiano mabao ya Nigeria yamefungwa na Rasheedat Busayo dakika ya 21 akipokea pasi ya Mary Imo aliyemvisha kanzu beki wa Tanzanite na kupiga shuti la mbali nje ya 18
  Kipa wa Tanzanite,  Wema Rashid (kulia) akiwa taabani leo baada ya kufungwa 6-0   
  Dakika 28 Rasheedat Busayo tena aliwainua vitini mashabiki wachache wa Nigeria waliokuwa uwanjani hapo baada ya kufunga bao la pili kwa shuti la mbali baada ya kipa wa Tanzanite kutoka langoni kwake na bao la tatu la Nigeria lilifungwa na Florence Ijamilusi dakika ya 36 akipokea pasi safi ya Mary Imo.
  Dakika ya 39 Nigeria walipata bao la nne kupitia Mary Imo kwa shuti kali linalomshinda kipa wa Tanzanite. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko ambapo Nigeria walikwenda wakiwa mbele kwa mabao 4-0.
  Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Tanzanite wakionekana kuamka na kutafuta bao lakini walishindwa kuendana na kasi ya wapinzani wao na kujikuta dakika ya 51 wakiruhusu kufungwa bao la tano kupitia Florence Ijamilusi. 
  Cynthia Pnyekidachi aliyeingia kuchukua nafasi ya Florence dakika ya 57 alihitimisha karamu ya mabao ya Nigeria akiifungia timu hiyo bao la sita bao lililodumu hadi dakika ya 90 ya mchezo huo
  Waamuzi wa mechi hiyo walikuwa Batol Ibrahim aliyekuwa mwamuzi mkuu akisaidiwa na Hanadi Mohamed na Remaz Osman wote kutoka nchini Sudan.
  Kikosi cha Tanzaniate kilikuwa; Wema Rashid, Gelwa Yona, Stella Wilbert, Aquila Gasper, Vero Gabriel, Esther Mayala, Asphat Kasindo, Rukia Anaph, Zainab Ati, Opa Clement na 
  Philomena Daniel.
  Nigeria; Oluwakemi Famuditi, Onyinyechukwu Okeke, Ewomizino Efit, Florence Ijamilusi, Grace Chinyere, Mary Imo, Glory Akumbu, Ope Yemi Anu, Amoo Bashrat, Lilian Tule na 
  Rasheedat Busayo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TANZANIA YATANDIKWA 6-0 NA NIGERIA KUFUZU KOMBE LA DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top