• HABARI MPYA

  Sunday, September 17, 2017

  OMOG AVUTIWA NA BAO LA BOCCO, TIMU KUONDOKA ALFAJIRI KUIFUATA MBAO

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mcamroon wa Simba SC, Joseph Marius Omog amemsifu mshambuliaji wake, John Raphael Bocco kwa bao zuri la tatu Simba ikishinda 3-0 dhidi ya Mwadui FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo baada ya mchezo huo, Omog alisema kwamba anashukuru kwa ushindi huo akicheza mechi ya tatu mfululizo bila kuruhusu nyavu zao kuguswa na wapinzani.
  Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi amefunga mabao mawili, lakini Omog amekunwa zaidi na bao la Bocco, akisema; “Nampongeza sana Bocco amefunga goli zuri sana, kwa kuwa tangu ametoka kwenye maumivu hajafanya vizuri, hivyo leo ni mwanzo wake mzuri,”amesema.
  John Bocco (kulia) leo amefunga bao zuri la tatu Simba ikishinda 3-0 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam

  Mashabiki wa Simba walizomea mabadiliko ya Omog mara mbili leo kwanza akimtoa Mghana Nicholaus Gyan na kumuingiza Mwinyi Kazimoto dakika ya 61 na baadaye akimtoa Kichuya na kumuingiza Mrundi, Laudit Mavugo dakika ya 65 wakionekana kabisa kutaka Bocco ndiye atolewe.
  Lakini Bocco akawaonyesha mashabiki wa Simba kwamba Omog alikuwa sahihi katika mabadiliko yake kwa kufunga bao la tatu dakika ya 72 kwa shuti la umbali wa mita 20 na zaidi pia. 
  Wakati huo huo: Kikosi cha Simba kinaondoka Jumanne Alfajiri kwa ndege ya ATC kwenda Mwanza kwa ajili ya mchezo wake ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Mbao FC.
  Beki Erasto Nyoni na viungo Haruna Niyonzima na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim waliokosa mechi ya leo na Mwadui kutokana na kuwa majeruhi, watasafiri keshokutwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OMOG AVUTIWA NA BAO LA BOCCO, TIMU KUONDOKA ALFAJIRI KUIFUATA MBAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top