• HABARI MPYA

  Wednesday, September 06, 2017

  NGASSA NA MBEYA CITY YAKE WAPANIA KUIPIGA NDANDA

  Na Mwandishi Wetu, MBEYA
  MSHAMBULIAJI mkongwe wa Mbeya City, Mrisho Khalfan Ngassa amesema watahakikisha wanaendeleza wimbi la ushindi katika mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ndanda FC Jumapili Uwanja wa Sokoine.
  Mbeya City ilianza na ushindi wa 1-0 dhidi ya Maji Maji ya Songea katika mchezo wake wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Agosti 26, mwaka huu Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
  Na Jumapili itarejea Uwanja wa nyumbani kujaribu kushinda mechi ya pili mfululizo, chini ya kaimu kocha wake Mkuu, Mohammed Kijuso kufuatia kuondoka kwa Mmalawi, Kinnah Phiri.
  Mrisho Ngassa amesema watahakikisha wanaendeleza wimbi la ushindi dhidi ya Ndanda FC Jumapili  

  Kuelekea mchezo huo, Ngassa ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online kwamba wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaibuka na ushindi dhidi ya Ndanda Jumapili ili wajiweke kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu.
  “Tumekuwa na maandalizi mazuri kabla ya msimu, na tumeendelea na maandalizi mazuri baada ya mechi yetu ya kwanza, hivyo ni matarajio yetu tutashinda huo mchezo,”alisema Ngassa. 
  Kwa ujumla Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea wikiendi hii, mechi nyingine za Jumapili zikiwa ni kati ya Singida United watakaokuwa wenyeji wa Mbao Uwanja wa Namfua, Mtibwa Sugar wataikaribisha Mwadui Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting  Uwanja wa Kaitaba, Bukoba na Lipuli wataikaribisha Stand United Uwanja wa Samora, Iringa.
  Awali ya hapo, Jumamosi Azam FC watakuwa wenyeji wa Simba Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na Tanzania Prisons wataikaribisha Maji Maji ya Songea Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGASSA NA MBEYA CITY YAKE WAPANIA KUIPIGA NDANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top