• HABARI MPYA

    Friday, March 10, 2017

    MAHAKAMA YAWASAFISHA MATANDIKA NA CHACHA TUHUMA ZA RUSHWA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam leo imewaachia huru Maofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) waliokuwa wanakabiliwa na tuhuma za kuomba rushwa ya Sh. Milioni 25 baada ya kuonekana hawana hatia.
    Hakimu Mkazi, Huruma Shahidi leo amewaachia huru wote Msaidizi wa Rais wa TFF, Juma Matandika na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa shirikisho hilo, Martin Chacha baada ya kubaini hawana kesi ya kujibu. 
    Juma Matandika na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa shirikisho hilo, Martin Chacha wameachiwa huru  

    Wawili hao walifikishwa mahakamani baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwatia hatiani kufuatia madai ya kurekodiwa wakiomba rushwa ya Sh. milioni 25 kutoka kwa viongozi wa Chama Cha Soka Geita (GFA) ili kuisaidia timu yao kupata nafasi ya kupanda Ligi Kuu Tanzania.
    Mapema baada ya shutuma hizo, Chacha alijiuzulu nafasi ya Ukurugenzi wa Mashindano TFF, wakati Matandika alisimamishwa kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi wa kesi hiyo. 
    Ilidaiwa Februari 4, mwaka jana viongozi hao wa GFA na klabu ya Geita Gold, Salum Kulunge na Constantine Morandi, walikwenda TFF kwa ajili ya kufuatilia rufaa kuhusu uhalali wa usajili wa mchezaji Mohammed Jingo wa timu ya Polisi Tabora, lakini kwa sababu timu ya Geita Gold Mine ilikuwa inachuana na Polisi Tabora kuwania nafasi ya kupanda Ligi Kuu kutoka Kundi C, wakashawishiwa na Maofisa hao wa TFF kutoa rushwa ya Sh. milioni 25.
    Ilielezwa washtakiwa waliomba rushwa kuishawishi TFF na Idara ya Uhamiaji Tanzania kutoa uamuzi wa Rufaa dhidi ya Polisi Tabora ili kuisadia Geita kupanda Ligi Kuu. Na baada ya kesi hiyo kuunguruma kwa takriban mwaka mmoja, leo watuhumiwa wote wameachiwa huru.
    Matandika anaweza kurejeshwa kazini moja kwa moja baada ya Mahakama kumsafisha, wakati Chacha anaweza kurudi iwapo tu yeye mwenyewe ataamua na TFF itakuwa tayari kumpokea tena. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAHAKAMA YAWASAFISHA MATANDIKA NA CHACHA TUHUMA ZA RUSHWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top