• HABARI MPYA

    Sunday, December 25, 2016

    ZAMUNDA: AFRICAN LYON NDIYO KIBOKO YA VIGOGO LIGI KUU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MMILIKI wa African Lyon, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ amesema kwamba wao ndiyo kiboko ya vigogo na watahakikisha msimu huu hawafungwi na timu yoyote kati ya Azam, Simba na Yanga.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online juzi baada ya kulazimisha sare ya 1-1 na mabingwa watetezi, Yanga, Kangezi alisema kwamba hawafanyi hivyo kwa kubahatisha bali ni kutokana na uwezo wao.
    “Kupata sare leo Yanga wamekuwa na bahati sana, ilikuwa tuwafunge lakini bahati nzuri wakachomoa,”alisema.
    Mmiliki wa Lyon, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ amesema kwamba wao ndiyo kiboko ya vigogo Ligi Kuu

    Kangezi alisema kwamba baada ya kuwasimamisha Yanga jana, wanaendelea na mechi zao za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mzunguko wa pili, lakini Simba wajipange.
    “Tumecheza na Azam wamebahatika kupata sare kama Yanga, ila tunasema Simba nao watie maji, wakati wao ukifika wajue wana pointi zetu tatu,”alisema.   
    Yanga juzi ilishindwa kurejea kileleni mwa Ligi Kuu baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na African Lyon jana jioni Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Matokeo hayo yaliifanya Yanga iendelee kukamata nafasi ya pili kwa pointi zake 37 baada ya kucheza mechi 17 sawa na Simba iliyo kileleni kwa pointi zake 38.  Simba inaweza kuongeza gepu la pointi hadi nne iwapo itashinda dhidi ya JKT Ruvu leo Uwanja wa Uhuru. 
    Lyon walitangulia kupata bao dakika ya 67 kupitia kwa Ludovic Venance aliyemalizia pasi ya mchezaji wa zamani wa Yanga, Abdallah Mguhi ‘Messi’ kabla ya Yanga kusawazisha dakika ya 74 kupitia kwa mkali wake mabao, Amissi Tambwe akimalizia krosi nzuri ya beki wa kulia Juma Abdul.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ZAMUNDA: AFRICAN LYON NDIYO KIBOKO YA VIGOGO LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top