• HABARI MPYA

  Jumamosi, Desemba 24, 2016

  SIMBA WAZIDI KUIACHA YANGA MBIO ZA UBINGWA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Simba SC imeendelea kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya jioni ya leo kuichapa JKT Ruvu bao 1-0 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Simba inafikisha pointi 42 baada ya kucheza mechi 17 sasa ikiwazidi kwa pointi nne mabingwa watetezi, Yanga SC ambao jana walilazimishwa sare ya 1-1 na Africam Lyon Uwanja wa Uhuru pia. 
  Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na Hans Mabena wa Tanga aliyesaidiwa na Omar kambangwa wa Dar es Salaam na Khalfan Sika wa Pwani, hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa bao hilo 1-0.
  Kiungo Muzamil Yassin akikimbia kushangilia baada ya kuifungia bao pekee Simba katika ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Ruvu jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 
  Kiungo Mghana wa Simba, James Kotei akimdhibiti mchezaji wa JKT Ruvu 
  Winga wa Simba, Shiza Kichuya akimtoka beki wa JKT Ruvu
  Beki wa Simba, Abdi Banda akipiga kichwa kuokoa mbele ya mchezaji wa JKT Ruvu
  Mshambuliaji wa Simba, Pastory Athanas akimtoka beki wa JKT Ruvu  

  Bao hilo lilifungwa na kiungo wake mahiri, Muzamil Yassin dakika ya 45, baada ya kazi nzuri ya Pastory Athanas.
  Awali, timu hizo zilishambuliana kwa zamu na utamu zaidi ulikuwa eneo la katikati ya Uwanja, ambako kiungo Hassan Dilunga wa JKT alikuwa anaonyeshana kazi na viungo wa Simba, Jonas Mkude na James Kotei kutoka Ghana.
  Mshambuliaji Pastory Athanas aliyesajiliwa dirisha dogo mwezi huu kutoka Stand United akicheza kwa mara ya kwanza leo alionyesha kiwango kizuri na kuwafurahisha mashabiki wa Simba.
  Na akicheza kama mshambuliaji pekee mbele ya lango la JKT, Pastory aliisumbua ngome ya timu hiyo ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na kukaribia kufunga mara kadhaa.
  Winga Shiza Kichuya kwa mara ya pili mfululizo leo alishindwa kufurukuta kutokana na kuwekewa na ulinzi mkali na mabeki wa JKT Ruvu.
  Kipa Mghana, Daniel Agyei alionyesha kiwango kizuri akiokoa michomo kadhaa ya hatari na kuizuia Simba SC kuruhusu bao.  
  Kikosi cha Simba kilikuwa: Daniel Agyei, Jonas Mkude, Janvier Bukungu/Hamad Juma dk50, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Method Mwanjali, Shiza Kichuya, James Kotei/Said Ndemla dk79, Pastory Athanas na Mohamed Ibrahim/Jamal Mnyate dk62. 
  JKT Ruvu: Hamis Seif, Salim Gilla, Michael Aidan, Frank Nchimbi, Yussuf Chuma, Kelvin Nashon, Edward Joseph, Hassan Dilunga, Hassan Materema, Mussa Juma/Kassim Kisengo dk80 na Ally Bilal/Atupele Green dk62.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA WAZIDI KUIACHA YANGA MBIO ZA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top