• HABARI MPYA

    Sunday, December 25, 2016

    WACHEZAJI WA YANGA KUDAI HAKI YAO SI VIBAYA, LAKINI SI KWA KUGOMA

    KWA siku mbili za mwanzo za wiki, wachezaji wa Yanga walikuwa wana mgomo na hawakufanya mazoezi Jumatatu na Jumanne.
    Mgomo huo ulikuwa maalum kushinikiza walipwe mishahara yao ya Novemba, ambayo kwa bahati mbaya ilichelewa.
    Na waligoma kuelekea mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya African Lyon uliofanyika Ijumaa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Baada ya kutotokea mazoezini na Jumanne pia, uongozi wa Yanga ukaingiwa woga na kuamua kutafuta suluhisho la mgomo wa wachezaji wake.
    Inaelezwa viongozi walizungumza na wachezaji na baada ya kuahidiwa kwamba watalipwa kabla ya Ijumaa siku ya mechi na Lyon, Jumatano wakarudi mazoeini.
    Walifanya mazoezi Jumatano jioni na Alhamisi asubuhi, baada ya kuwa hawajafanya mazoezi tangu wacheze na JKT Ruvu Jumamosi ya wiki iliyopita na kushinda 3-0.
    Haikuwa ajabu walipocheza kwa kiwango cha chini katika mchezo dhidi ya Lyon na kulazimishwa sare ya 1-1 Ijumaa Uwanja wa Uhuru.
    Walipogoma kufanya kwa siku mbili za Desemba kwa sababu ya mishahara ya Novemba, wakarejea baada ya kuahidiwa kulipwa kabla ya Ijumaa.
    Na bila shaka walilipwa kabla ya kuingia kwenye mchezo na Lyon – na vipi kuhusu siku mbili ambazo hawakufanya kazi wakiwa wamegoma, watakatwa katika mishahara ya Desemba, au?
    Lakini kwa kugoma kufanya mazoezi siku mbili, wachezaji wa Yanga walimkomoa nani - ambaye mazoezi hayo yangemjenga zaidi ya wao wenyewe?
    Kweli mishahara ilichelewa, lakini kwa kuwa ni haki yao wamelipwa, wangelipwa au watalipwa tu hata kwa kufungua kesi Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
    Hivi wachezaji wa Yanga wanajua mashabiki wangapi wa timu yao walikwenda uwanjani siku hiyo wakiwa hawajalipwa mishahara hiyo hiyo ya Novemba, na wengine hata miezi zaidi?
    Zipo namna nyingi za wachezaji wa Yanga au timu yoyote kuwasilisha ujumbe wa kudai maslahi yao, lakini si kwa kugoma.
    Msimu uliopita Ligi Kuu ya Ghana ilikumbwa na msukosuko mkubwa wa kiuchumi baada ya kupoteza udhamini na klabu nyingi ziliyumba na kushindwa kujimudu, kiasi cha kushindwa kulipa mishahara, lakini wachezaji hawakugoma.
    Wachezaji wa Yanga wanajua mara ya mwisho ni lini wachezaji wa African Lyon walilipwa mishahara?
    Si vibaya wachezaji kudai haki zao, ikiwemo mishahara au posho zinapochelewa, lakini kugoma kwa kweli si jambo zuri, kwa sababu madai yote hulipwa hata baada ya muda mrefu kiasi gani.
    Wakati umefika, wachezaji wa Tanzania na nchi jirani wanaocheza nchini sasa wabadilike na kuonyesha kwamba wanajitambua kwa kuachana na mambo ya kienyeji.
    Wamegoma kufanya mazoezi, kwanza wameathiri hali zao wenyewe kimchezo na matokeo yake wakaingia kichovu katika mechi dhidi ya Lyon na kuponea chupu chupu kufungwa.
    Lakini pia kwa kugoma kwao wameiathiri timu imepoteza pointi mbili katika mchezo ambao ilitarajia kabisa kushinda ili kujiweka pazuri katikaa mbio za ubingwa.
    Kilichotokea wiki hii ni kitu cha aibu kwa wachezaji wa klabu kubwa kama Yanga ambao dhahiri hadi kufika hapo, wamepitia changamoto nyingi. Kudai haki zao si tatizo, lakini kugoma si kwa kugoma.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WACHEZAJI WA YANGA KUDAI HAKI YAO SI VIBAYA, LAKINI SI KWA KUGOMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top