• HABARI MPYA

    Thursday, December 29, 2016

    AZAM YATHIBITISHA KUWAMWAGA WASPANIOLA, CHECHE APEWA TIMU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    AZAM FC imetangaza rasmi kuachana na makocha wake kutoka Hispania chini ya Zeben Hernandez Rodriguez leo na kwamba kocha wa vijana, Iddi Nassor 'Cheche' ataiongoza timu kwa muda akisaidiwa na Iddi Abubakar.
    Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba amesema leo kwamba kwamba wamefikia makubaliano na makocha hao kutoka Hispania kuvunja mikataba.
    Jopo hilo la makocha linaundwa na Kocha Mkuu Zeben Hernandez, Msaidizi wake, Yeray Romero, Kocha wa Makipa Jose Garcia, Kocha wa Viungo, Pablo Borges na Mtaalamu wa tiba za Viungo, Sergio Perez.
    Iddi Cheche (kushoto) sasa ndiye atakaimu ukocha wa Azam wakati timu ikitafuta kocha mwingine

    Kawemba amesema kwamba uamuzi huo umefikiwa na Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo jana, na umetokana na mwenendo mbaya wa Azam FC kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo imefikia raundi ya pili hivi sasa.
    "Azam FC inawatakia kila la kheri na mafanikio mema makocha hao huko waendako na inawashukuru kwa mchango wao wote walioutoa kwenye timu kwa kipindi chote walichokaa, ikiwemo kuwapa taji la kwanza la Ngao ya Jamii mwaka huu kwa kuifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2,"amesema Kawemba.
    Amesema wakati uongozi ukiwa katika mchakato wa kusaka kocha mpya, kikosi hicho kitakuwa chini ya makocha wa timu ya vijana ya timu hiyo, Idd Cheche na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar, ambao walianza kazi jana jioni kukiandaa kikosi kuelekea mchezo wa leo dhidi ya Tanzania Prisons.
    "Azam FC inapenda kuwaambia mashabiki wake kuwa wawe watulivu katika kipindi hiki kwani uongozi umefanya uamuzi sahihi kwa ajili ya kuinyanyua timu juu ili hatimaye ushiriki wetu wa michuano mbalimbali uweze kuwa ni wa kiwango cha juu tofauti na hali ilivyokuwa sasa," amesema Kawemba.
    Hernandez anaondoka Azam FC akiwa ameingoza timu hiyo kwenye mechi 18 rasmi ambazo ni za mashindano, 17 za ligi na moja ya Ngao ya Jamii, amefanikiwa kushinda mechi nane, sare sita na kufungwa mara nne.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM YATHIBITISHA KUWAMWAGA WASPANIOLA, CHECHE APEWA TIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top