• HABARI MPYA

  Alhamisi, Desemba 29, 2016

  SIMBA NA RUVU LEO UHURU, CHAMAZI NI AZAM NA PRISONS

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaendelea leo kwa michezo miwili tu kuchezwa mjini Dar es Salaam.
  Uwanja mkongwe kabisa Jijini, Uhuru vinara wa ligi hiyo, Simba wataikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani, wakati Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Azam watakuwa wenyeji wa Prisons ya Mbeya.
  Azam wataingia kwenye mchezo wa leo siku moja baada ya taarifa za kufukuza benchi zima la Ufundi la makocha kutoka Hispania na kumrejesha mchezaji wake wa zamani, Kali Ongala kuiongoza timu. 
  Simba SC wako vizuri, chini ya kocha wa zamani wa Azam FC, Joseph Marius Omog na wanataka kuendeleza wimbi la ushindi leo Uhuru.
  Mapema tu kabla ya kuanza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, kocha Omog alisema wamerejea kuendeleza kazi nzuri waliyofanya mzunguko wa kwanza wakimaliza wanaongoza.
  Na Omog anasema anataka wawe juu hadi mwisho wa msimu na ili kutimiza lengo hilo, lazima wapigane kwa nguvu zao zote kila mechi washinde.
  Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alisema jana kwamba wamekuja Dar es Salaam kwa lengo moja tu, kuifunga Simba.
  Simba iko juu ya timu zote kwenye msimamo wa Ligi Kuu kutokana na pointi zake 41 za mechi 17, ikifuatiwa na Yanga SC yenye pointi 40 za mechi 18. 
  Ruvu Shooting inashika nafasi ya sita kwa pointi zake 23, ilizovuna kwenye mechi 17.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA NA RUVU LEO UHURU, CHAMAZI NI AZAM NA PRISONS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top