• HABARI MPYA

  Jumatatu, Desemba 26, 2016

  SIMBA KUMALIZANA NA NDUSHA, ANGBAN JUMATANO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imesema kwamba hadi kesho itakuwa imekwishawalipa kipa Vincent Angban na kiungo Mussa Ndusha ili waondoke Alhamisi kuerejea kwao.
  Angban kutoka Ivory Coast na Ndusha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wote wameachwa Simba SC katika dirisha dogo mwezi huu, kufuatia kusajili kwa Waghana, kipa Daniel Agyei na kiungo James Kotei.
  Baada ya kusitishiwa mikataba, wawili hao wanapaswa kulipwa na Simba SC kulingana na vipengeel vya mikataba yao.
  Na akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online leo, Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele amesema kwamba klabu haina tatizo na wachezaji hao na tayari wamefikia makubaliano juu yaa namna ya kumalizana.
  Mussa Ndusha (kushoto) aliichezea Simba mara ya mwisho ikifungwa na Mtibwa Sugar 2-1 Desemba 12, mwaka huu

  Kahemele alisema kwamba wachezaji wote hao wana uelewa mzuri na wanaielewa vizuri mikataba waliyosaini kujiunga na Simba, hivyo hakuna tatizo lolote baina yao.
  “Hatuna tatizo nao kabisa, tumezungumza nao vizuri na tumefikia makubaliano kwamba tutakuwa tumekwishamalizana nao hadi kufika Jumatano (kesho) ili Alhamisi waondoke,”alisema.
  Aidha, Kahemele alisema wanauheshimu na kuuthamini mchango wa wachezaji hao kwa kipindi cha kuitumikia Simba na wanawatakia kila laa heri waendako.
  Wakati huo huo: Kikosi cha Simba jana kimeendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting Alhamisi wiki hii.
  Kahemele alisema kwamba timu imeweka kambi hoteli ya Spiece, Mnazi Mmoja mjini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo huo. 
  “Tangu tutoke Mtwara tuliweka kambi Spiece na tutaendelea kuwa hapo hadi baada ya mchezo huu na Ruvu Shooting tutakapokwenda Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi,”alisema Kahemele.
  Simba SC imeuanza vyema mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kushinda mechi mbili mfululizo za mwanzo na kuzidi kupaa kileleni.
  Wekundu hao wa Msimbazi walianza kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara kabla ya kuilaza 1-0 JKT Ruvu katikaa mchezo uliofuata Jumamosi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Matokeo hayo yanawafanya Wekundu wa Msimbazi wafikishe pointi 41 baada ya mechi 17, wakiwazidi kwa pointi nne, mabingwa watetezi, Yanga wanaofuatia katika nafasi ya pili kwa pointi zao 37. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA KUMALIZANA NA NDUSHA, ANGBAN JUMATANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top